WAKALA wa Jiolojia Tanzania (GST), umetoa ufafanuzi juu ya tetemeko
lililotokea mkoani Kagera na kusema kuwa kitovu cha tetemeko hilo, kiko
chini ya ardhi urefu wa kilometa 10. Aidha umetoa tahadhari kwa wananchi
kwa kuzingatia na kuepuka madhara, yanayoweza kusababishwa na tetemeko
la ardhi kabla ya tukio, wakati wa tukio na baada ya kutokea tukio ili
kupunguza madhara yanaweza kutokea.
Katika taarifa yake jana, wakala huyo alisema kuwa tetemeko hilo
lililonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi, limetokana na
misuguano ya mapande makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi
mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa.
“Tetemeko hilo lililotokea Septemba 10 mwaka huu majira ya saa 9:27,
mchana kitovu chake kilikuwa kati ya latitudo 10 06’ na longitudo 31055’
eneo ambalo ni kilomita 20 Kaskazini Mashariki mwa kijiji cha Nsunga na
kilomita 42 Kaskazini Magharibi mwa mji wa Bukoba, alisema Mtendaji
Mkuu wa GST.
“Nguvu za mtetemeko wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli
ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara
makubwa,” alisema Mtendaji Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma.
Alisema kutokana na ukubwa huo maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera,
ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa ikiwa ni
kusababisha vifo vya watu 16 kuharibika kwa nyumba nyingi, watu wengi
kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za nyumba.
Aidha taarifa hiyo ilisema kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi
liko karibu na mkondo wa Magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki
inakisiwa kuwa mtetemo huo ulisababishwa na kuteleza na kusuguana kwa
mapande ya miamba juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.
Aidha alisema mpaka sasa Tanzania na duniani kote, hakuna vifaa au
taratibu za kuweza kutabiri utokeaji wa matetemeko ya ardhi na vifaa
vyote na taratibu zote za kuratibu au kupima matetemeko ya ardhi
vinapima ukubwa na tabia ya tetemeko baada ya tetemeko kutokea.
Alisema wakala huyo tayari umepeleka wataalamu katika eneo la tukio ili
kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo na kwamba
miongoni mwa vituo vya jiolojia vilivyorekodi tukio hilo la tetemeko ni
kile cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu sana na eneo la tetemeko
hilo.
Mtendaji Mkuu alisema jamii inapaswa kupewa elimu ya tahadhari ili kila
mmoja aelewe nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni
pamoja na kupata mafunzo kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu
namna ya kuhudumia majeruhi ama wahanga na pia jeshi la zima moto ili
kupata elimu kuhusu namna ya kutumia kizimamoto.
Alisema wananchi wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa
kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa
ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa
kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo.
Wakati wa tetemeko mamlaka hiyo imesema kuwa wananchi wanashauriwa kukaa
mahali salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti
mirefu na miinuko mikali ya ardhi. Pia ilisema watu wanashauriwa kukaa
nje ya nyumba katika sehemu za uwazi.
“Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae chini
ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na pia
ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili
kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo,” ilieleza taarifa hiyo ya Profesa
Mruma.
Aidha ilisema baada ya kutokea tukio la tetemeko wananchi wanashauriwa
kuzima umeme katika majengo ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme
kama mitetemo itaendelea.
Pia wametakiwa kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama
hayakupata madhara na kama yanaweza kuendelea kutumika na ikibidi uwaita
wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi. Waathirika waomba msaada
Katika hatua nyingine waathirika wa tetemeko hilo wameiomba serikali
kuwasaidia kuwajenga mahema kwa ajili ya kujihifadhi, baada ya nyumba
zao kuanguka kutokana na tetemeko hilo.
Mmoja wa waathirika hao, Joyce Ndukeke alisema kuwa tangu wamepatwa na
janga hilo hawajapata msaada na kuwa wanachokifanya ni kujikusanya
pamoja na kulala nje. Ndukeke ambaye ana watoto wanne alisema kuwa
wakati tetemeko hilo likitokea alikuwepo nyumbani pamoja na watoto wake
huku mumewe akiwa safarini kikazi.
"Nyumba zetu zimeanguka hatujapata msaada, hatuna pa kulala tunalala nje
na watoto, lakini sasa tuna hofu zaidi maana hata jana (Jumapili)
limepita tena, tunaomba tusaidiwe kujengewa mahema maana huu ni msimu wa
mvua inaweza kunyesha wakati wowote tukanyeshewa pamoja na vitu vyetu
tulivyofanikiwa kuokoa vikaharibika," alisema.
Pia muathirika mwingine, Mutalemwa Emmanuel alisema kuwa kutokana na
janga hilo wanaendelea kuogopa hata kwenda kutafuta vyumba vya kuishi
katika nyumba nyingine maana nyumba nyingi zina nyufa na kutokana na
tetemeko kupita kwa mara nyingine, wanahofia hata nyumba hizo zinaweza
kuanguka.
Alisema hata kwa wale ambao nyumba zao bado zimesisimama hawawezi kwenda
kuomba hifadhi humo maana nyingi zina nyufa, tetemeko limepita tena
mara mbili baada ya lile la Jumamosi ingawa ni kwa kiwango kidogo si
kubwa kama la kwanza, kwa hiyo wanahofia na nyumba zenye nyufa zinaweza
kuangua. Alimwomba Rais John Magufuli kuwasaidia kupata msaada wa haraka
angalau kuwapatia mahema ya kuishi maana sasa wanalala nje.
Wakati wananchi hao wakitoa malalamiko hayo ya kutopata msaada wowote,
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro aliwataka wananchi hao kuwa
na subira kidogo maana serikali inaendelea kufanya kila jitihada ili
kuhakikisha wanapata msaada wa haraka.
"Sasa imeundwa kamati ya kufuatilia wananchi waliopatwa na janga hilo,
ili kujua hasara iliyotokana na tetemeko hilo lakini pia kubaini misaada
ya haraka inayohitajika kwa kila mmoja, tunaendelea na vikao lakini
katika wilaya yangu tunakadiria watu zaidi ya 3,000 ndiyo hawana
makazi," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema kuwa
hakuna vifo vilivyoongezeka, na kwamba majeruhi waliolazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamepungua kutoka 253 hadi 61. Kuhusu dawa na
vifaa tiba vingine vinavyohitajika alisema hakuna upungufu na kuwa
huduma zinaendelea kutolewa kwa majeruhi wote.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye
alisema kuwa watu hao wanahangaika sana kwani wanalala nje kwahiyo ni
vizuru serikali kwa kushirikana na wadau mbalimbali na taasisi wakatoa
msaada huo wa halaka ili kuondoa adha hiyo.
Pia aliwashauri wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia damu
katika hospitali ya rufaa ili kuifanya benki ya damu kuwa na damu ya
kutosha kwani majeruhi wanahitaji damu na kwamba viongozi wa chama hicho
wamejitoa kwa ajili ya kuchangia damu katika Hospitali ya Mkoa huo
pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Omumwani ambayo inamilikiwa
na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni