MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Taifa, Augustine Mrema
amewapongeza wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), kwa kuamua kuacha kususa kuhudhuria vikao vya Bunge kushinikiza
Naibu Spika, Tulia Ackson ajiuzulu au aondolewe kwenye wadhifa huo.
Mgomo huo ulisababisha wabunge wa Ukawa kutoshiriki kwenye Bunge la
Bajeti, jambo ambalo limesababisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha
2016/2017 ipitishwe bila wabunge wa upinzani kuijadili na kuchangia
mawazo yao bungeni.
Kwa mujibu wa barua yake kwenda kwa Spika wa Bunge Job Ndugai, Mrema
ameeleza athari ya mgomo huo wa Ukawa kuwa ni kusababisha bajeti ya
serikali ipitishwe kwa mawazo ya upande mmoja wa chama tawala.
Aidha, ilieleza kwamba mawazo ya wananchi kutoka kwenye majimbo
yanayoongozwa na wabunge wa Ukawa yalikosekana, hivyo kuwafanya wabunge
hao kuwanyima haki wapiga kura wao, kwa kuwakosesha uwakilishi kwenye
Bunge la Bajeti.
“Bunge la bajeti ni kikao nyeti kwa vile linajadili na kupitisha mapato
na matumizi ya serikali kwa mwaka husika, ambayo yanamhusu na kumgusa
kila mwananchi, hivyo haikuwa busara kwa wabunge wa Ukawa kususa vikao
vya Bunge la Bajeti na kuwafanya wapiga kura wao wakose uwakilishi
kwenye kikao nyeti kama hicho,” alisema. Mrema alisema, kuwepo kwao
bungeni kungeweza kusaidia kuboresha bajeti hiyo kutokana na michango
yao ya mawazo ambayo wangeyatoa na kupata bajeti bora zaidi kwa manufaa
ya taifa.
“Sisemi kwamba bajeti iliyopitishwa ni mbaya, lakini kuwepo kwa wabunge
wa upinzani kungesaidia kuboresha ili iwe nzuri zaidi kwa manufaa ya
wapigakura wao waliowachagua majimboni mwao,” alisema.
Alisema “Hata kama Naibu Spika alikuwa na kasoro katika utendaji wake wa
kazi, lakini Ukawa hawakupaswa kususa vikao vya bunge hilo, badala yake
wangetafuta ufumbuzi wa suala kwa kufuata njia za kikatiba na kisheria,
ikiwemo kutumia kanuni za Bunge.”
Alisema kwa kususa vikao vya Bunge, Ukawa wamesababisha madhara makubwa
kwa wananchi hususani wapigakura wao ambayo hawawezi kulipika na
wanaweza wakawaadhibu kwa kosa hilo kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka
2020, kwa sababu wananchi waliwachagua ili kwenda kuwawakilisha bungeni
na si kwenda kususia vikao vya Bunge.
“Sisi TLP tunaona kwamba Ukawa wamedhoofisha upinzani badala ya
kuimarisha upinzani kama wenyewe wanavyodai, kwani huwezi kuimarisha
upinzani kwa kususia vikao vya Bunge hususani Bunge la Bajeti,” alisema.
Alisema Ukawa wanapaswa kujifunza kwamba kususa vikao si mwarobaini wa
kutatua mgogoro ya kisiasa, bali migogoro ya kisiasa hutatuliwa kwa
kupitia njia za vikao na mazungumzo. Hata hivyo, alisema madhara
yaliyopatikana kutokana na mgomo huo hayawezi kulipika kwa sababu Bunge
la Bajeti limeshapita na haliwezi kurudiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni