Tafiti ambazo zimewahi kufanywa na wanasoikolojia mbalimbali kuhusu
maisha ya mwanadamu na mazingira yake hususani suala zima la mafanikio,
zilitoa majibu ya kwamba maisha ya mwanadamu yanaathiriwa kwa kiwango
kikubwa na vitu vikubwa viwili ambavyo ni;
Jambo la kwanza ni kuishi kwa kukariri.
Suala hili ndilo ambalo limekuwa limeathiri maisha ya wengi kwa asilimia
kubwa sana. Watu wanashindwa kuishi kulingana na jinsi ambavyo dunia
inakwenda kasi.
Hebu tunawatazame wafanyabiashara wangapi ambao leo hii ambao walianza
kufanya biashara tangu muda mrefu kabla ya kukua kwa teknolojia hususani
masuala ya mitandao ya kijamii ambao leo hii wanatumia mitandao hiyo ya
kijamii katika kuzitangaza bidhaa au huduma zao?
Kimsingi ukifanya tathimini utagundua ni wachache sana. Unajua ni
kwanini wapo wachache? kwa sababu wameshazoea na kuishi maisha ya
kukariri huku wakiamini ya kwamba kutumia mitandao ya kijamii ni suala
gumu kwao.
Hii ni ishara ya kwamba imani waliyonayo ni ngumu sana ambayo hawawezi
kubadilika hata kupelekea wao kutokuamini ya kwamba wanaweza kujitangaza
kupitia mitandao ya kijamii. Imani waliyonayo ni kwamba kutumia
mitandao ya kijamii ni suala la kupoteza muda.
Lakini ukweli haupo hivyo ndugu yangu mwenye tabia kama hizo, tambua na
elewa ya kwamba kuna watu ambao inabidi wakutambue kwa shughuli ambayo
unaifanya ambao kimsingi wanaishi mbali na sehemu ulipo.
Ewe mfanyabiashara acha kuishi kimazoea na kuamini ya kwamba mahali
ulipo sasa panatosha, ila amini ya kwamba ipo haja leo ya kujua ya
kwamba wapo baadhi ya wadau wanapenda kujua hicho ambacho unakifanya.
Jambo la Pili ambalo linaathiri Maisha ya wengi ni kuishi kimazoea.
Kuishi kimazoea ndiko kunakotufanya tuishi kwa manung'uniko na
masikitiko hasa katika maisha haya ya kila siku. Hebu tazama kwa mfano
utawala huu wa awamu ya tano jinsi ambavyo unafanya kazi kila mmoja kwa
nafsi yake moyoni ana yake ya kusema, unajua ni kwanini kwa sababu watu
wengi tulikwisha kuzoea kuishi maisha ya kimazoea sana, hivyo tunajikuta
kwa asilimia kubwa tunashindwa kuendana na kasi hiyo na tunabaki
tunalalamika kwa sababu tulishazoea kuishi kimazoea.
Kuishi kimazoea ni kubaya sana mpenzi msomaji wa makala haya kwa sababu
pindi changamoto yeyote ijitokezapo kwetu huwa ni kikwazo kikubwa cha
kuweza kulifikia lengo. Leo hii ukimkuta mtu ambaye anafanya jambo
fulani na ukamshauri afanye jambo jingine atakataa, unajua ni kwanini
atakataa? atakataa kwa sababu amezoea kufanya jambo lake la awali hivyo
kubadili kufanya jambo jingine kwake hutengeneza hofu ya kushindwa.
Ndugu yangu ambaye kwa hali yeyote ile unataka kufanikiwa, na si
kufanikiwa tu, bali kufanya mafanikio yako yamguse kila mmoja wetu kwa
namna moja ama nyingine hakikisha ya kwamba usiishi katika misingi
ambayo ni ya kukariri au kuishi katika mtazamo wa kimazoea, kwani
kufanya hivi ni kujiua mwenyewe.
Nakusihi tena kwa kukumbusha ujio wako hapa dunia si kwa bahati mbaya
ila ni kwa kusudio maalum amini ya kwamba wewe ni zaidi ya matajiri
wakubwa waliopo sasa, pia tumia muda mwingi kumshukuru Mungu kwa kukupa
hekima na akili ya kuweza kufikiri, pia muombe akupe ujasiri wa kuweza
kutenda mambo kwa fikra na mitazamo chanya
Chanzo: Muungwana blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni