Simba inatarajia kujitupa dimbani tena Jumamosi ya wiki hii kuumana na
Azam FC lakini tayari imegundua ni sekta gani Azam wanaweza kuitumia
kuwazidi ujanja, hivyo tayari imejipanga kuhusiana na hilo.
Simba imejinadi kuwa itapambana na timu hiyo kusaka ushindi kwa udi na
uvumba lakini imebaini kuwa Azam inaweza ikabebwa kwa kutumia faida ya
nyasi za bandia zilizopo katika Uwanja wa Uhuru, Dar watakaoutumia
katika mchezo huo.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amefafanua kuwa wanafahamu
ugumu wa mechi hiyo kutokana na sababu ya kung’anga’nia kukaa kileleni,
hivyo itakuwa kama fainali ingawa wanahisi wapinzani wao watakuwa na
faida na nyasi za uwanja, hivyo nao wanajua wafanye nini siku hiyo.
“Mechi itakuwa ngumu, wote tuna pointi 10 na tuna idadi sawa ya mabao ya
kufunga na kufungwa. Wao wanahitaji ushindi kama ilivyo kwetu
tunavyouhitaji kwa nguvu zote. Tunafahamu pia wao wamezoea nyasi bandia,
tofauti na sisi, hivyo hicho kinaweza kuwa kikwazo kwetu.
“Lakini kama benchi la ufundi tunajua tutafanya nini na hakuna
kitakachoharibika, tutalizingatia hilo katika mazoezi yetu na mbinu
tutakazojifunza katika maandalizi yetu ya mechi hiyo,” alisema Mayanja
raia wa Uganda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni