ZIARA ya kimataifa aliyoifanya Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Marekani, Ulaya, Canada na Umoja wa
Mataifa kulalamikia uvurugaji wa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba mwaka jana,
imeanza kuzaa matunda
Tayari taasisi ya kimataifa ya umoja wa wanaliberali – Liberal
International (LI) – imeliandikia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa
Mataifa (UNHRC) kutaka kutolewa kwa vikwazo dhidi ya Serikali ya
Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana kwenye tovuti ya LI, taasisi hiyo
imetaka baraza hilo lenye jukumu la kulinda misingi ya haki za binadamu
kwenye mataifa yote wanachama wa UN, kuchukua hatua kali ili kukomesha
“uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukandamizaji wa haki za kisiasa
na kiraia visiwani Zanzibar.”
Katika tamko walilolitoa na kufikishwa mbele ya Mkutano wa 33 wa Baraza
hilo uliofanyika Septemba mosi mwaka huu, Liberal International imetaka
jumuiya ya kimataifa, kufikiria kuweka vikwazo vya kusafiri na kuzuia
mali za watu wote walioshiriki kuidhinisha vitendo vya utesaji wanasiasa
wa upinzani na wafuasi wao.
Taasisi hiyo ambayo CUF ni mwanachama wa muda mrefu, imetoa wito kwa
wabunge wanaofuata mtizamo wa kiliberali walioko upande wa serikali na
upinzani katika mataifa yote duniani kuchukua msimamo imara kupitia
mabunge ya nchi zao na kutoa matamko ya kupinga walichokiita “uonevu
wanaofanyiwa viongozi wa upinzani Zanzibar na wafuasi wao.”
“Tunaitaka serikali ya Zanzibar na Tanzania kuheshimu utawala wa sheria
na kuingia katika majadiliano na upinzani ndani ya muda maalum hatua
ambayo itawezesha kuundwa serikali ya mpito na kukubali kuitishwa kwa
uchaguzi mpya ili kuondoa mgogoro uliojitokeza baada ya kufutwa kwa
uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015,” imesema taarifa ya LI.
Hatua hiyo ya LI kuandikia Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa
Mataifa inakuja wiki kadhaa baada ya Maalim Seif kukutana na taasisi
mbalimbali za kimataifa zinazoshughulikia maendeleo ya demokrasia na
utawala bora, pamoja na wakuu wa serikali za Marekani, Ulaya na Canada.
Maalim Seif aliyefuatana na baadhi ya wasaidizi wake pia alifika
Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya The Hague, Uholanzi ambako aliwasilisha
malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa Zanzibar kwa
idhini ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hatua ya Maalim Seif na CUF imekuja baada ya CCM kumuamuru Jecha Salim
Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi
mkuu wa Zanzibar, 28 Oktoba, baada ya kubaini kuwa chama hicho
kimepoteza madaraka kupitia sanduku la kura.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni