Ibada ya hijja imemalizika rasmi katika mji wa Makkah na Madina na
mahujaji wa dini ya kiislamu zaidi ya milioni 2 kutoka nchi zipatazo 164
wameanza kurejea makwao walikotoka.
Ibada ya mwaka huu imekuwa ya mafanikio kwa kumalizika salama. Hii ni
kutokana na Serikali ya Saudi Arabia kuwa na mipango madhubuti kwa
kuimarisha miundombinu, usafiri, ulinzi na usalama na kurekebisha dosari
zilizojitokeza mwaka jana.
Maeneo ya misikiti yote miwili ya Makkah na Madina yaliimarishwa na
yanaendelea kujengwa ikiwa ni pamoja na kupanuliwa ili kuongeza nafasi
za kutosha kufanyia ibada.
Mahujaji kutoka Tanzania wapatao 2,000 wako salama na wao ni miongoni
mwa walioshiriki katika ibada na sasa wako njiani kurejea Tanzania.
Hatua zilizochukuliwa na mamlaka za ulinzi za Saudi Arabia ni pamoja na
kuhakikisha kuwa makundi ya misafara ya mahujaji hayagongani kati ya
wanaokwenda na wanaorudi, njia mbalimbali zilikuwa zikifungwa na
kufunguliwa ili kuruhusu misafara kwenda uelekeo mmoja bila kukutana.
Hatua hii ilisaidia kuepusha ajali kama iliyotokea wakati wa ibada ya
hijja ya mwaka 2015.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni