WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea michango wa zaidi ya sh. bilioni 1.4
kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya
Wafanyabiashara wa Kitanzania kwa ajili ya kusaidia wananchi
waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera.
Tetemeko
hilo lilitokea Jumamosi, 10 Septemba, 2016 na kusababisha vifo vya watu
17 hadi leo na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya
wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264
zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.
Akizungumza
katika hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia wahanga hao
jana Jumanne, 13 Septemba, 2016 Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango
yao ya fedha na vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji. Amesema
tetemeko hilo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
Alisema
tetemeko hilo limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili za
sekondari za Nyakato na Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na
tetemeko hilo.
“Serikali
itajitahidi kuhakikisha inarejesha miundombini iliyoharibiwa na
tetemeko hilo katika kipindi kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine
waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka
tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu, Jenista Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo
cha maafa kufanya thamnili kujua athari zilizosababishwa na tetemeko
hilo.
Mawaziri
wengine walioko mkoani Kagera wakiendelea kufanya tathmini hiyo ni
pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako.
Alisema
Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya
Maafa ya mkoa wa Kagera imefungua akaunti maalumu katika benki ya CRDB
kwa ajili ya kupokea michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za
akaunti hiyo ya Kamati ya Maafa ya Kagera ni CRDB 0152225617300.
Pia
Waziri Mkuu aliwapongeza na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kuamua
kutoa posho zao za kikao cha jana kwa ajili ya kuchangia wahanga wa
tetemeko hilo na kuwaomba wananchi wengine kujitokeza na kutoa michango
yao.
Wakati
huo huo viongozi wa makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil
wameahidi kujenga shule mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa
ya miundombinu yake imeharibika vibaya. Shule hizo zitajengwa katika
kipindi cha siku 30.
Hafla
hiyo iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na
Biashara, Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Balozi, Dk. Aziz Mlima.
Chanzo: Mpekuzihuru.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni