Kurasa

Jumanne, 13 Septemba 2016

Mahakama kutoa uamuzi malalamiko kesi mauaji ya dadake Msuya


 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itatoa uamuzi wa malalamiko ya washtakiwa wa mauaji ya dada wa bilionea Erasto Msuya, mnamo Septemba 27.

Mahakama ilipanga kutoa uamuzi huo jana baada ya kusikia majibu ya hoja za upande wa mashtaka.

Washtakiwa katika kesi hiyo, Miriam Stephen Mrita (41) na mfanyabiashara Revocatus Evarist Muyela (40) wanadaiwa kumuua kwa makusudi Anathe Msuya, kwa kumchinja, nyumbani kwake, Kibada Kigamboni Mei 25, 2016.

Miriam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo alikuwa mke bilionea Msuya. Bilionea Msuya aliuawa kwa risasi Agosti, 2015 eneo la Mijohoroni, kando ya Barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Washtakiwa hao kupitia kwa Wakili wao Peter Kibatala wamedai kuwa walikubali kosa hilo baada ya kuteswa na polisi na kulazimishwa kukubali.

Mbele ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Magreth Bankika, Wakili Kibatala amedai kuwa washtakiwa hao wana vielelezo vya mateso waliyoyapata ikiwamo kuvimba miguu na majeraha ya mwili.

Kutokana madai hayo, ameiomba Mahakama iamuru uongozi wa Magereza kuwafanyia uchunguzi wa afya na matokeo ya uchunguzi huo yawasilishwe mahakamani na kuwekwa katika kumbukumbu.

Hata hivyo, upande wa  mashtaka umepinga madai hayo na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo ameieleza Mahakama kuwa shtaka linajitosheleza kiasi kwamba washtakiwa wanaelewa kile wanachoshtakiwa.

Wakili Lukondo amedai kuwa si kweli kwamba waliteswa na  kama ingekuwa hivyo, wangefuata taratibu na kwamba uongozi wa Magereza hauwezi kumtibu mtu ambaye hana Fomu namba tatu ya Polisi (PF3).
Chanzo: Ubuyublog.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni