Kwa
jinsi binadamu tulivyo, tunaweza kuona vitu vyote ambavyo havionekani
mbele ya macho yetu. Ukifuatilia kwa undani unagundua kuwa vitu ambavyo
tunaambiwa na kuamini kuwa havionekani, kiuhalisia vitu vyote vyaweza
kuonekana endapo ukiamua. Kwa mazoea, wengi tunafikiri kwamba kama kitu
hakionekani mbele ya macho yetu ya kawaida, basi tunasema hakipo.
Ajabu
na kweli ni kwamba, mtu asipoona kitu kwa macho yake ya kawaida, basi
usidhani kwamba kitu hicho hakionekani na wengine ufikiri kwamba kitu
hicho hakipo kabisa duniani. Kumbuka kuwa kuendelea kufikiri na kuamini
kwamba kitu fulani hakionekani au hakipo haina maana kwamba hakionekani
kwa wengine! Wewe usipoona wengine wanaona.
Tunapodhani
kwamba kitu fulani hakipo duniani, wakati kipo, moja kwa moja
tunapoteza uwezo wetu wa ndani na nje wa kukifanya kile kisichoonekana
kionekane mbele ya macho ya wengi.
Kwa
binadamu ni akili yake pekee iliyo na uwezo wa kuona vitu vyote
vinavyoonekana na visivyoonekana. Unapofikiri kwa kutumia akili
(ubongo), hapo tunasema kuwa umeona kwa macho ya akili au ubongo. Pia,
kile uonacho kupitia fikra zako, ndicho ambacho hukusukuma wewe kutumia
rasilimali zilizopo, ili kukiweka katika uhalisia.
Kitu
kikishakuwa kwenye uhalisia, basi hapo tutasema “umefanya kwa vitendo
au umetenda”. Ukisha tenda, maana yake ni kwamba, unakifanya kile
ambacho kilikuwa hakionekani mbele ya macho yetu ya kawaida, kionekane
sasa machoni mwa wengi. Endapo watu wataona kile ulichotenda,
wasijidanganye kuwa “wameona bali wajue wametazama”.
Kuna tofauti kubwa sana kati ya “kuona” na “kutazama”.
Kutazama siyo kuona, na kuona ni zaidi ya kutazama. Dhana nzima ya
“KUONA” ni pale tunapoweza kutumia akili kuota ndoto, halafu tukapiga
picha, halafu tukapanga, tukaamini, na kisha tukatenda.
Kwa
maana nyingine ni kwamba, akili (ubongo) ni kiwanda na karakana ya
kuzalisha mambo mapya. Lakini pale tuonapo picha ya kitu kutokea nje
(kwa macho ya kawaida), basi huko siyo “kuona” bali ni “KUTAZAMA”.
Binadamu
wengi tunao uwezo wa kuona kila kitu endapo tunataka kufanya hivyo.
Pamoja na uwezo mkubwa tuliopewa, bado hatuutumii katika kuona fursa za
kujiondoa kwenye majanga ya umaskini.
Watu
waliofanikiwa mara nyingi wanatwambia kila siku kuwa popote tulipo
Tanzania tumezungukwa na fursa nyingi. Kwanini sasa watu wengi ni
maskini katika nchi iliyo na fursa nyingi? Jibu ni moja tu nalo ni “watu wengi hawaoni fursa bali wanatazama fursa”.
Utajiri
wa uhakika hautapatikana kutokana na watu wengi kutazama fursa BALI ni
pale tu watu watakapoweza kutumia akiri zao kuona fursa na kisha kuanza
kuchukua hatua za maksudi ili kuzifikia fursa hizo.
Kumbe watu wengi tumekuwa ni watu wa “kutazama” fursa na siyo “kuona” fursa.
Unapoona fursa unakuwa na ujasiri, nguvu na shauku ya kutenda ili
kufaidi fursa husika. Lakini unapotazama fursa, mara nyingi unajawa sana
na uoga, hofu inayotokana na wewe kukosa majibu muafaka ya maswali
unayojiuliza baada ya kuona kwa macho yako kile kilichofanywa na
wenzako.
Unapotazama
kitu kilicho mbele ya macho yako, mara nyingi utajiuliza maswali mengi
bila majibu juu ya jinsi kilivyotengenezwa. Unapokosa majibu sahihi ya
maswali yako, mara nyingi utapata hitimisho moja tu! Nalo ni
“HAIWEZEKANI”.
Ukishajiridhisha
kuwa haiwezekani, basi unaamua kwenda kutazama fursa nyingine ambayo
nayo utapata hofu na woga wa kuifanyia kazi. Mwisho wake unaishia kuwa
ni mtu wa kutazama na kuongea tu! Huku ukizidi kuandamwa na maisha ya
taabu na umaskini.
Watu
wenye kuona fursa ndio wenye “maono”. Maono ni ndoto kujumlisha na
ukweli wa mambo. Ukiwa na maono yafanyie kazi. Tumia macho ya akili au
ubongo kuona fursa.
Ukitumia
macho ya ubongo au akili, utaweza kuona vinavyoonekana na
visivyooekana. Fursa za uhakika hazionekani kwa macho ya kawaida.
Usipoona
fursa machoni mwako haina maana kwamba fursa hizo hazipo! ni uamuzi
wako tu! ukiamua zionekane na ziwepo basi, itakuwa hivyo.
Lakini,
ukiamua zisiwepo basi, hazitakuwepo wala hazitaonekana mbele ya macho
yetu ya kawaida. Jambo hili aliwahi kulisisitiza mwanafalsafa wa
Kifaransa aliyejulikana kama Henri Bergson kuwa “Jicho linaona kile ambacho akili iko tayari kukiona au kuelewa”
Kutokana
na maneno hayo ya Bwana “Henri Bergson”, tunajifunza kwamba fursa
ambazo hazionekani machoni mwako, ni lazima uziite wewe mwenyewe ndipo
zitakuja kwako na usipofanya hivyo watu wengine watafanya hivyo, mwisho
wake fursa ulizotakiwa kuzifaidi wewe, utabakia KUZITAZAMA kwa jirani.
Endapo
jirani au watu wengine wasipoziita fursa hizo, basi zitaendelea kubakia
katika hali yake hiyo ya kutoonekana, mpaka zitakapoitwa na vizazi
vijavyo.
Leo
hii Tanzania kama taifa tunaishi maisha duni kutokana na ukweli kwamba
watu wengi wanaanzisha miradi ya biashara baada ya kutazamia kwa
wengine. Ni bora ukaona mradi anaoufanya mwingine kuliko kuutazama.
Watu
wengi hasa Tanzania, huwa hawaoni miradi bali huitazama tu basi. Kwa
maana nyingine ni kwamba, unapoona mwenzako akijishughulisha na mradi
fulani wa kibiashara na wewe ukafanya kama anavyofanya bila kuongeza
kitu chochote kipya, basi ujue kuwa mradi huo “haujauona” BADALA yake “umeutazama” tu!.
Ni nini faida za kufanya mradi ambao umeuona?
Kimsingi
nchi inapokuwa na watu wengi ambao tunafanya miradi tunayoiona kwa
macho ya ubongo au akili zetu, ni wazi kwamba tutakuwa na uwezo mkubwa
wa kutatua changamoto na kero nyingi ambazo zinasababisha maisha magumu
kwa jamii tunayoishi nayo.
Pili,
tutaweza kutengeneza bidhaa na huduma za thamani kubwa kwa watu wa
Tanzania na dunia kwa ujumla. Tatu, tutasaidia katika kuharakisha ukuaji
wa uchumi wetu binafsi na taifa letu kwa ujumla.
Watu
wengi tukiona na siyo kutazama miradi ya maendeleo, tutaweza kutegeneza
bidhaa nyingi ambazo ni tofauti tofauti. Tukiwa na bidhaa nyingi zenye
ubora wa hali ya juu, ni wazi kwamba tutaweza kuvuta pesa nyingi kutoka
kwa watu wengine hasa nje ya nchi. Watu wenye pesa zao, watapenda watume
pesa zao kwetu, ili kupata bidaa na huduma na hivyo kutufanya sote tuwe
na pesa nyingi.
Kwa
ngazi ya kitaifa ni kwamba watu kutoka mataifa ya nje watapendelea
kutuma pesa zao Tanzania ili kununua suruhisho tulizonazo juu ya
changamoto walizonazo kwao – hali hii ndiyo itachangia uwepo wa ajira na
hatimaye nchi kuwa na uchumi mkubwa.
Hili tuwe na uwezo wa kuona miradi tufanye nini?
Katika
hili hakuna namna na hakuna njia muafaka zaidi ya kuzidi kuwekeza sana
kwenye fikra. Ninaposema kuwekeza kwenye fikra ni zaidi ya watu kusoma
hadi vyuo vikuu au kubobea kwenye taaluma fulani.
Uwekezaji
mzuri kwenye fikra ni ule ambao unajifunza kila siku kwa kutumia njia
mbalimbali, kama vile kujenga tabia ya kuwa mdadisi wa kila jambo/kitu
na hasa yale yanayohusu kile ambacho unakifanya au unatarajia kukifanya.
Kabla
ya kuanzisha mradi wako hakikisha unafanya utafiti wa kero na
changamoto zinazowakabili watu waliokuzunguka au wengine wa mbali ---
kwa kawaida kero inayo wapata watu waliokuzunguka mara nyingi huwa
inawapata pia watu wengi walioko mbali na wewe.
Uzuri
wa uwekezaji katika fikra hauna usumbufu na wala hauhitaji gharama
kubwa. Kinachohitajika ni nidhamu ya kufanya kile ulichopanga kukifanya
hata kama ni kigumu. Kwahiyo, huu ni uwekezaji ambao unaweza kufanywa na
karibu wa aina yoyote, ilimradi mtu awe anajua kusoma na kuandika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni