Kurasa

Jumamosi, 8 Oktoba 2016

DUCE: Hata kama waziri asingewafukuza, tungewafukuza

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako  
Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce), Profesa William Anangisye amesema wangechukua hatua za kuwafukuza wanafunzi walioonekana kwenye video wakimshambulia mwanafunzi huko Mbeya

Wanachuo hao waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo, Frank Msigwa na John Deo kwa kushirikiana na Sanke Gwamaka wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere walionekana wakimshambulia Sebastian Chinguku wa Shule ya Sekondari ya Kutwa Mbeya.

Profesa Anangisye amesema kitendo walichokifanya ni cha kinyama na kimekiuka maadili ya ualimu na kwamba kwa mujibu wa taratibu za taaluma hiyo, mwalimu mkuu ndiye mwenye mamlaka ya kumuadhibu mwanafunzi.

“Tunalaani kitendo walichokifanya wanafunzi wetu kimetutia aibu. Hata kama Serikali isingechukua hatua, uongozi wa Duce tusingeweza kuvumilia unyama huo. Tungewatoa maana tayari wamekiuka miiko ilhali tulikuwa tukiwaandaa kuwa walimu,” amesema.

Baada ya tukio hilo kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya habari, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza kuwatimua chuoni akisema kitendo hicho ni kosa la jinai.

Hata hivyo, wiki mbili zilizopita, wahadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa, Dk Hellen Myeya na Anneth Kasebele waliwakagua wanafunzi hao lakini hawakupata malalamiko yoyote wala kugusiwa kama kuna tatizo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni