Dodoma. Serikali imetangaza kuanza utafiti kujua viashiria na matokeo ya Ukimwi katika ngazi ya kaya utakaofanyika mwezi ujao.
Utafiti huo utakaofanyika nchini kote, una lengo la kuiwezesha Serikali
kupanga mipango endelevu ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.
Akizungumza mjini hapa jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye alisema utafiti huo utahusisha kaya
16,000 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy, matokeo ya utafiti huo yataeleza hali halisi ya maambukizi ya VVU ilivyo nchini.
Waziri huyo alikuwa akifunga mafunzo ya wasimamizi na wadadisi wa
utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania, yaliyofanyika katika
Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini hapa.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kipindi chote cha utafiti ili kufanikisha mpango huo.
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa siku 49, yalihusisha jumla ya wauguzi 187
kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani na kusimamiwa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu.
Waziri Ummy aliwaomba wakuu wa kaya zitakazohusika katika utafiti kutoa
ushirikiano ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango endelevu ya
kupambana na Ukimwi nchini.
Alisema taarifa zote zitakazotolewa na kukusanywa katika utafiti huo
zitabaki kuwa siri kwa kuwa wadadisi watakaoifanya kazi hiyo wamekula
kiapo cha maadili cha kutunza siri.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa alisema lengo
la utafiti huo ni kutathmini ukubwa wa tatizo la Ukimwi nchini, kiwango
cha utumiaji wa huduma za kujikinga na maambukizi, tiba kwa waathirika
pamoja na huduma zinazoendana na mapambano ya Ukimwi.
“Pia, utafiti huu utajikita katika kubaini kiwango cha maambukizi mapya
katika ngazi ya kitaifa, CD4, homa ya ini pamoja na huduma nyingine
zinazohusiana na Ukimwi ikiwamo kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto,” alisema Dk Chuwa.
Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard
Maboko, aliwataka wadadisi hao kuwa waadilifu wakati wa kukusanya
taarifa.
chanzo: muungwana.co.tz
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni