Ni wazi nabii hakubaliki kwao kwani awali kabla ya Uchaguzi Mkuu
wa mwaka jana kufanyika wananchi na baadhi ya viongozi walinukuliwa
wakisema kwa hali ilivyo na nchi ilipofikia inahitaji kiongozi mwenye
maamuzi magumu atakayeweza kuweka mambo kwenye mstari kwani ni dhahiri
baadhi ya mambo yalianza kwenda mrama.
Tangu kuapishwa kwake Novemba 5, mwaka jana tayari Rais Magufuli amekaa
madarakani kwa takribani miezi 10 na siku 10 hadi hii leo akiwa tayari
amefanya mambo kadhaa yenye tija kwa taifa ikiwemo operesheni tumbua
majipu ambayo imerejesha nidhamu ya kazi na kukuza uwajibikaji na
uaminifu kwa wafanyakazi wa umma.
Kama ambavyo wazungu husema “wherever there is positive there must be
negative” pamoja na mengi mazuri yaliyofanywa hadi sasa na Rais Magufuli
aliyekuwa Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
chini ya mwavuli wa Ukawa Edward Lowassa ameibuka na kusema licha ya
kwamba serikali iliyopo madarakani inafanya vizuri lakini suala la
ukandamizaji wa demokrasia ni tatizo kubwa ambapo lisiposhughulikiwa
mara moja litaleta madhara makubwa kwa taifa.
Kuhusu suala la elimu Lowassa amesema suala la elimu bure halikupaswa
kuanzia na uchangiaji madawati badala yake maslahi ya walimu
yangezingatiwa kwanza ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara baina ya
waalimu na serikali kutokana na ulimbikizaji wa stahiki zao. Akasema
kama angekuwa rais jambo la msingi katika sekta ya elimu ambalo
angeshughulikia mara moja ni mishahara ya waalimu na maslahi yao kwa
ujumla badala ya kuhangaika na madawati.
Kuhusu operesheni Ukuta ambayo inatarajiwa kufanyika Oktoba Mosi baada
ya kuahirishwa Septemba Mosi ili kupisha viongozi wa dini na serikali
kutafuta suluhu ya hatma ya ukandamizaji demokrasia nchini, Lowassa
amesema kama muafaka hautapatikana wataona namna ya kufanya ili uhuru wa
demokrasia uzingatiwe nchini kwa kuwa anaamini demokrasia ni kukaa meza
moja na kukubaliana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni