MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imewahukumu wakazi wa mtaa wa
Nsemlwa Manispaa ya Mpanda, Godfrey Mabuga na Rashid Ramadhani, kifungo
cha miaka 20 jela.
Wamepewa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na vipande
vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 48 .
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa baada ya kuridhika na
ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka huku ikimwachia huru
mshtakiwa wa tatu.
Baada ya kusomewa hukumu hiyo, Mabuga na Ramadhani waliangua kilio
mahakamani hapo huku mshtakiwa aliyeachiwa huru akipiga magoti na
kuonesha ishara ya msalaba.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ntengwa alisema mahakama hiyo imewatia
hatiani watuhumiwa hao kupitia Kifungu Namba 86 (1) na (2) cha Uhifadhi
wa Wanyamapori ya mwaka 2009 na Kifungu Namba 57 (1) cha Sheria ya
Uhujumu Uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2000.
Awali, Mwendesha Mashitaka, Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi,
Jamira Mziray alidai washitakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Mei
20 mwaka 2014, katika eneo la mtaa wa Fisi kata ya Majengo Manispaa ya
Mpanda.
Alidai siku hiyo ya tukio, walikamatwa na vipande vinne vya meno ya
tembo vyenye thamani ya Sh milioni 48 ambayo ni sawa na tembo wawili
hai.
Katika utetezi wake, Mabuga aliiomba mahakama imwachie huru kwa kile
alichodai kuwa hakutenda kosa hilo, bali alisingiziwa tu na askari wa
Mamlaka ya Hifadhi za taifa (Tanapa) na polisi waliomkamata.
Alidai kuwa siku hiyo alikuwa Usevya Tarafa ya Mpimbwe wilayani Mlele.
Hata hivyo, alipotakiwa kuonesha tiketi ya gari la abiria alilosafiria,
kama sehemu ya ushahidi wake mahakamani hapo, alishindwa kuionesha.
Chanzo:Muungwana.co.tz
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni