VIONGOZI wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Kaliua mkoani Tabora,
wamemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad akae
pembeni kama ameshindwa kuongoza chama hicho.
Walisema hayo wakati wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Mpilipili kata ya Ugunda wilayani humo.
Walisema hawatambui maamuzi ya kusimamishwa uanachama aliyekuwa
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mbunge wa Kaliua,
Magdalena Sakaya.
Mwenyekiti wa CUF wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya
kitongoji cha Mpilipili, Lubaga Lubaga, alisema wao kama wilaya bado
wanawatambua viongozi hao.
Lubaga alibainisha kuwa kinachofanyika ndani ya chama hicho kwa sasa ni
usanii wa Maalim Seif, hivyo wakiwa kama wanachama halali wa chama hicho
Kaliua wataendelea kupingana naye.
“Maalim Seif kwanza hana msaada wowote kwani hata alipokuwa kwenye
serikali ya mseto iliyopita visiwani Zanzibar hakuwa na msaada wowote na
mkoa wa Tabora, hivyo kama ameshindwa kuongoza CUF akae pembeni,”
alisisitiza Lubaga.
Alisema hawajaona kosa lolote alilofanya mbunge wao, Sakaya.
Alisisitiza wao bado wanamtambua Sakaya kuwa ni mwakilishi wao bungeni.
Kuhusu maamuzi ya kumteua Julius Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa muda wa CUF,
alisema hatua hiyo ni kukiuka Katiba ya chama chao na inaonesha dhahiri
kuwa sasa ndani ya chama hicho, kuna mchezo mchafu unaofanywa kwa
maslahi ya watu wachache.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Tuombe Mungu, Abdulrahaman Toni
alisema CUF wilaya ya Kaliua, bado wako imara na wanawaunga mkono
Profesa Lipumba na Sakaya, hivyo maamuzi yaliyofanywa dhidi ya viongozi
hao ni batili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni