Wakati mwanamfalme
wa Kiafrika na karani mmoja mwanamwali Mzungu wa maisha ya wastani
kutoka kwa wamiliki wa bima wa Lloyd, walipoamua kuoana mnamo mwaka
1948, ilichochea hisia mbalimbali nchini Uingereza na Afrika.
Seretse Khama alikutana na Ruth Williams alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Oxford na wakaanza kuchumbiana.Baada ya masomo yake, alitarajiwa kwenda nyumbani hadi katika taifa lake lililokuwa koloni ya Uingereza wakati huo ikijulikana kama Bechuanaland ambayo sasa ni Botswana, na kuoa mmoja wa watu wa kabila lake, lakini mapenzi yake kwa Williams ya libadilisha kila kitu.
Familia yake ilipinga ndoa hiyo na Khama akalazimika kukatalia mbali fursa ya kuwa mfalme.
Serikali ya Uingereza iliingilia kati na kujaribu kupinga ndoa hiyo haua iliyomfanya Khama kufukuzwa kutoka nchi yake.
Askofu wa London, William Wand, angeruhusu tu harusi inayofanyika kanisani ikiwa tu utawala nchini Uingereza ungeruhusu ndoa hiyo kufanyika. Hilo halikufanyika.
Wapenzi hao wawili walilazimika kuoana baadaye katika ofisi ya mwanasheria mkuu iliyoko Kensington huko London mnamo Septemba mwaka 1948.
Waziri mkuu wa Afrika Kusini wakati huo Daniel Malan, alitaja ndoa yao kama "iliyojaa kichefuchefu" huku mwanafunzi mmoja aitwaye Julius Nyerere, ambaye baadaye alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, akasema "ni mojawepo ya hadithi nzuri sana za mapenzi duniani",
Mmoja wa walioshuhudia alizungumza na dadake Ruth Williams, ambaye alisema harusi hiyo ilikuwa "mapenzi yaliyoshinda chuki".
Wawili hao walipata uungwaji mkubwa huku maandamano yakizidi huko Bechuanaland, kushinikiza kutambuliwa kwa ndoa hiyo ambapo baadaye walikubaliwa kurejea nchini humo mnamo mwaka 1956 baada ya watu wa kabila la Bamangwato, lake Bw Khama, walipoamua kutuma barua kwa njia ya telegram hadi kwa Malkia Elizabeth wa II.
Kufanikisha uhuru
Seretse Khama aliamua kukatalia mbali utawala wa kabila lake na akaamua kuwa mkulima na mfugaji huko Serowe. Baadaye alikibuni chama cha Bechuanaland Democratic Party na akashinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 1965.Akiwa Waziri mkuu wa Bechuanaland (Botswana) alifanikisha nchi hiyo kujipatia uhuru mwaka 1966 na akawa Rais wa kwanza wa Botswana.
Ruth Williams Khama, alifahamika kama Lady Khama baada ya uhuru na alihudumu kama mkewe Rais wa Botswana kuanzia mwaka 1966 hadi 1980.
Walijaliwa watoto wanne: Wa kwanza Jacqueline aliyezaliwa Bechuanaland mwaka 1950; Ian aliyezaliwa England mwaka 1953, na pacha Anthony na Tshekedi waliozaliwa Bechuanaland waliozaliwa 1958.
Ian Khama ndiye Rais wa sasa wa Botswana na alianza kuongoza mwaka 2008.
Ian na Tshekedi ni wanasiasa nchini humo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni