
Mahujaji wakutupa vijiwe kuashiria kupiga mawe shetani
Waislamu ulimwenguni kote wanasherehekea sikuukuu ya Eid Ul Hajj.
Mahujaji wamefika Mina leo Jumatatu(12.09.2016) kwa kutekeleza utaratibu
wa kumpiga mawe shetani,kaida ya mwisho kuu ya Hijja ya kila mwaka.Eneo hilo hata hivyo lilitokea mkanyagano na kusababisha maafa makubwa mwaka jana.
Utaratibu wa kupiga mawe shetani unafanywa mara tatu katika muda wa siku zijazo.
Mahujaji wakutupa vijiwe kuashiria kupiga mawe shetani
Mara ya kwanza inakuja mwanzoni mwa sikukuu ya Eid l-Adha, ambayo ni leo
siku ya kuchinja, siku ambayo ni takatifu kwa Waislamu, siku
inayoadhimishwa na zaidi ya Waislamu bilioni 1.5 duniani kote.Hatua kadhaa za usalama zimechukuliwa kuepusha kutokea tena kwa maafa yaliyotokea mwaka jana, ambayo yalisababisha kiasi ya watu 2,300 kufariki wakati wakiingia katika daraja la Jamarat kutekeleza kaida hiyo ya kurusha vijiwe kama ishara ya kumpiga shetani, tukio linalofuatia hatua ya nabii Ibrahim kumpiga vijiwe shetani wakati akimtaka asitekeleze amri ya Mwenyezi Mungu ya kumchinja mwanawe Ismail.
Al-Kaaba , mahujaji wakizunguka al-Kaaba mjini Makka
Mahujaji hutupa vijiwe walivyovikusanya kutoka katika eneo la karibu la Muzdalifah siku ya Jumapili jioni dhidi ya kuta zilizojengwa kuwa kama ishara ya shetani.
Usalama waimarishwa
Mfalme wa Saudi Arabia Salman aliwasili Mina siku ya Jumapili kuhakikisha mahujaji wanatekeleza kaida hiyo "bila matatizo, kwa utulivu na usalama", shirika rasmi la habari la Saudia liliripoti.
Pia alifahamishwa kuhusiana na matayarisho kwa ajili ya mahujaji kupita kwa usalama kati ya Muzdalifah na Mina.
Baada ya kumrushia vijiwe shetani , kondoo huchinjwa na nyama kugawiwa kwa Waislamu ambao hawana uwezo na masikini, ikionesha kuwapo tayari kwa nabii Ibrahim kumtoa mwanae Ismail kwa amri ya Mwenyezi Mungu amchinje, ambapo baadaye alitolewa kondoo badala ya kijana huyo katika dakika ya mwisho.
Kaida ya kutupa vijiwe inafuatia hatua za nabii Ibrahim kukataa vishawishi vya kutomtii Mwenyezi Mungu kutoka kwa shetani.
Mkanyagano na maafa
Mkandagano wa mwaka jana ulikuwa mbaya mno katika historia ya Hijja.
Saudi Arabia inaendelea kusisitiza kwamba watu waliofariki ni 769, lakini tarakimu zilizokusanywa kutoka kwa maafisa katika zaidi ya nchi 30 zinatoa idadi ya juu mara tatu zaidi.
Maafisa wametangaza kuanzisha uchunguzi kuhusiana na maafa hayo lakini hakuna kilichotangazwa hadi sasa kutokana na uchunguzi huo. Hatua kadhaa za usalama zimeanzishwa mwaka huu.
Miongoni mwa hizo ni kuanzisha utaratibu wa kuvaa bangili maalum, ambayo huhifadhi data za binafsi za kila hujaji. Barabara pia zimepanuliwa katika eneo la Jamarat, magazeti ya nchi hiyo yameripoti.
Lakini hatua hizo mpya za usalama zilishindwa kuridhisha mahujaji wa kishia kutoka Iran , nchi ambayo ilikasirishwa mno na maafa hayo kwa kuwa ilipoteza mahujaji wengi katika mkasa huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusuf , Saumu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni