Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Kamati yake ya
Maudhui imekifungia kituo cha Redio 5 Arusha kwa kipindi cha miezi
mitatu pamoja na kukitoza faini ya sh. Milioni 5 kwa kosa la kukiuka
baadhi ya Kanuni za Huduma za Utangazaji (maudhui) kupitia kipindi chake
cha Matukio kilichorushwa Agosti 25, 2016.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, katika kipindi hicho Mbunge wa
Jimbo la Arusha Mjini Mh. Godbless Lema alitamka maneno ya kashfa
yaliyolenga kumdhslilisha Rais John Magufuli na serikali kwa ujumla.
Wakati akisoma maamuzi ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Maudhui Joseph Mapunda, aliongeza kuwa kituo hicho pia kilirusha maneno
yaliyo tamkwa na Lema ambayo yalikuwa yakihamasisha wananchi kushiriki
katika maandamano ya Ukuta yaliyopigwa marufuku na Jeshi la Polisi.
“Maneno ya Lema yalilenga kuhaasisha wananchi kupambana na jeshi la
polisi na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa
Taifa,” amesema.
Mapunda amesema uamuzi huo umetolewa na kamati hiyo baada ya kamati hiyo
kusikiliza maelezo ya utetezi yaliyotolewa na wa Uongozi wa Redio 5
Arusha.
“Baada ya kusikiliza maelezo ya utetezi kamati imeridhia kuwa kipindi
cha matukio kilikiuka baadhi ya kanuni za maudhui namba 5(a,b,c,d,f,h)
6(2) (b, c) na 18 (1) (b),” amesema.
Ameongeza kuwa ” kituo hicho kinatozwa faini ya sh. Milioni 5 ambazo
zitatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kuanzia leo, kinafungiwa kwa miezi 3
na kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa muda wa Mwaka 1 baada ya
kipindi cha kufungiwa kumalizika, “
Hata hivyo, Mapunda amesema haki ya wahusika kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo iko wazi ndani ya siku 30 kuanzia leo.
Kwa upande wa kituo cha redio cha Magic Fm ambacho nacho pia kwa mujibu
wa kamati hiyo kinadaiwa kukiuka kanuni za maudhui kupitia kipindi chake
cha Morning Magic kipengele cha Paka Rangi ambapo kilirusha maneno
yanayodaiwa kumkejeli rais na wananchi, kimepewa onyo kali pamoja na
kutakiwa kuomba radhi kwa muda wa siku tatu mfululizo.
“Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi
yaliyotolewa na Uongozi wa Magic Fm Redio, Kamati ya Maudhui imeridhika
kuwa kipindi cha Morning Magic kilikiuka baadhi ya kanuni za huduma za
utangazaji 2005. Kamati ya maudhui inaamua kutoa onyo kali kwa Magic
Radio, ” amesema na kuongeza.
“Pia inatakiwa kumuomba radhi Rais John Magufuli, wasikilizaji na
wananchi kwa ujumla. Tangazo la kuomba radhi litolewe kwa siku tatu
mfululizo katika taarifa za habari za saa 10.00 alasriri, na 3.00 usiku
kuanzia tarehe 17,9,2016.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni