Kurasa

Jumamosi, 8 Oktoba 2016

China: 'Ukinunua iPhone 7 umejifuta kazi!'

 Wateja wakiwa na iPhone 7 China

 Baadhi ya kampuni China zimetishia kuadhibu wanaonunua iPhone7
 

Kampuni kadha nchini Uchina zimetoa onyo kali kwa wafanyakazi wake na kuwataka wasinunue simu mpya ya kampuni ya Apple, iPhone 7.
Kampuni zilizotoa marufuku hiyo zinasema ni kwa sababu za kizalendo.
Nyingine zimesema zinataka kuwafunza wafanyakazi wake kutopenda sana raha na anasa za dunia.
  • Simu mpya ya iPhone 7 isiyotumia headphone
Kampuni ya dawa ya Nanyang Yongkang Medicine, katika mkoa wa Henan, ni moja ya zilizoagiza wafanyakazi wake kutonunua simu za iPhone 7 au Iphone 7 Plus.
"Ukivunja agizo hili, njoo moja kwa moja hadi afisini na utukabidhi barua yako ya kuacha kazi," ilani kutoka kwa kampuni hiyo iliyotumwa kwa wafanyakazi inasema.



Ilani iPhone 7s 
  Baadhi ya wafanyakazi wanasema barua ya kampuni hiyo inakiuka haki za wafanyakazi
Sera hiyo imetangazwa wakati sambamba na siku ya maadhimisho ya miaka 85 tangu wanajeshi wa Japan walipovamia maeneo ya mashariki mwa China mwaka 1931.
"Septemba 18 ni siku ya kihistoria. Msisahau tulivyodhalilishwa kama taifa. Hebu tususie bidhaa kutoka nje ya nchi," ilani kutoka kwa kampuni hiyo iliongeza.
Tovuti moja imemnukuu msemaji wa kampuni ya Nanyang Yongkang Medicine kwa jina Bw Liu akisema lengo la agizo hilo ni kuwahamasisha pia wafanyakazi kuangazia zaidi familia badala ya vitu vya anasa.
Barua hiyo ilisambazwa sana katika mitandao ya kijamii CHina, na kitambulisha mada "Wafanyakazi watakaonunua iPhone7 kufutwa" kilivuma katika mtandao wa Weibo.
Baadhi ya watu kwenye Weibo hata hivyo wameeleza kwamba kususia iPhone7 huenda kukawa kunawadhuru Wachina wenyewe kwani uzalishaji wa simu za Apple hufanywa katika viwanda vya kampuni ya Foxconn nchini Uchina.
Kwenye Weibo kumesambazwa pia picha za barua ya hospitali ya Fuling Xinjiuzhou Gynecology Hospital mjini Chongqing ambayo inawaonya wafanyakazi wasinunue iPhone7.
Barua hiyo inasema: "iPhone 7 imeanza kuuzwa sokoni na bei yake ni ya juu mno ukilinganisha na simu nyingine. Ili kuendeleza utamaduni kwa kutopenda matumizi ya anasa na kutumia pesa kwa busara, wasimamizi wa hospitali wamefikia uamuzi wa kuwapiga marufuku wafanyakazi wetu wasinunue simu za iPhone7."
Barua hiy inaongeza kwamba wanatakaokiuka agizo hilo hawatapewa alama za juu katika utathmini wa utendaji kazi wao.
Aidha, watahimizwa kurejesha simu hizo madukani.
Meneja wa hospitali hiyo ameambia BBC Trending kwamba hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mfanyakazi mmoja kununua iPhone 7 ilhali inajulikana kwamba bei ya simu hiyo ni mara tatu mshahara wake.
"Sipingi bidhaa kutoka nje lakini sipendi watu wakinunua simu ambazo bila shaka hawawezi kumudu kifedha. Baadhi ya watu hukopa pesa benki au kutoka kwa jamaa na marafiki, na wengine hata huuza viungo vyao kununua iPhone. Sitaki wafanyakazi wangu wafanye mambo kama hayo," amesema.
Baadhi ya watu wanaotetea uzalendo wa Wachina wamekuwa pia wakipinga simu za iPhone kuonyesha kutoridhishwa kwao na uamuzi wa jopo la kimataifa uliosema China haina haki ya kumiliki visiwa ambavyo imekuwa ikidai katika bahari ya South China Sea. Rais Barack Obama aliitaka China kutii uamuzi huo.

iphone Baadhi ya watu waliharibu simu zao za iPhone kuonyesha uzalendo
Video za watu wakiharibu iPhone zao kuonyesha uzalendo zimevuma sana mtandao wa Weibo.
Baadhi ya maduka China pia yamekataa kuuza simu za iPhone7 kama sehemu ya kususia bidhaa kutoka Marekani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni