Mwonekano wa radi baada ya kupiga.
SHINYANGA watu wawili wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakati wakiwa wamejikinga mvua chini ya mti kando ya malambo ya kunyweshea mifugo katika kijiji cha Ntundu, Kata ya Busangi katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 8.30 mchana katika kijiji hicho wakati mvua ilipokuwa ikinyesha, ndipo watu hao waliamua kujikinga kwenye mti na radi ikapiga na kusababisha vifo hivyo.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Fikiri Paschal (35) na Maneno Luzalia (16), wakati waliojeruhiwa na kupata mshituko baada ya radi kupiga ni watano ambao ni Mhoja Pasian (32), Abeli Feleshi (12), Nhungwa Jeremiah (22), Juma Mussa (16) na Paschal Mabula (11) ambaye ni mwanafunzi wa Ntundu.
“Waliopigwa radi ni watu saba ambao walikuwa wamejikinga mvua chini ya mti, kati yao wawili walikufa papo hapo na wengine watano walijeruhiwa na kukimbizwa kupatiwa matibabu katika zahanati ya Busangi na hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Kamanda Jumanne.
Aliwataka wananchi kutokaa karibu na miti, hasa kipindi hiki mvua za masika zinapokaribia kuanza kunyesha kwa wingi ili kuepuka tukio kama hilo, ambalo limepoteza maisha ya watu wawili, huku akifafanua kuwa katika mfumo wa umeme ni rahisi kupata madhara, hivyo ni vema wakachukuwa tahadhari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni