Serikali imejiandaa kurudia kukusanya maoni ya wananchi ili
kukamilisha muswada wa sheria ya ndoa ili kukamilisha kubadilika kwa
sheria hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Ijumaa hii bungeni mjini Dodoma, na waziri wa
katiba na sheria, Dk Harrison Mwakyembe, akijibu swali lililouliza
kuhusu kurejeshwa bungeni kwa muswada huo kwaajili ya kuufanyia
marekebisho.
“Sheria ya ndoa ya mwaka 71 ni matokeo ya mjadala mpana na shirikishi
kupitia walaka wa serikali namba moja wa mwaka 69. Lengo la mjadala huo
lilikuwa ni kupata muafaka kuhusu maudhui ya sheria hiyo ambayo inagusa
imani, mila na desturi za watanzania,” alisema Mwakyembe.
“Baada ya miaka zaidi ya 20 kupita tangu sheria hiyo ya ndoa itungwe,
serikali kupitia tume ya kurekebisha sheria iliifanyia mapitio sheria
hiyo na kubaini maeneo kadhaa yenye udhaifu na hivyo kuhitaji kufanyiwa
marekebisho. Kutokana na maoni ya tume wizara ya mambo ya katiba na
sheria iliandaa mwaka 2008 waraka wa baraza la mawaziri uliokuwa na
mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya ndoa ya mwaka 71,” alisisitiza.
“Kwa kuzingatia chimbuko la sheria hiyo, baraza liliiagiza wizara
kuandaa waraka maalumu wa serikali ya white paper ili kupata mjadala
mpana na shirikishi kama ilivyokuwa awali. Mapema mwaka 2010 wizara
ilikamilisha maandalizi ya waraka huo kubainisha hoja za wananchi
walizotakiwa kuzitolea maoni,” aliongeza.
“Serikali inalazimika kurudia taratibu za awali kususanya maoni ya
wananchi na kufanyia marekebisho sheria ya ndoa na kwamba mchakato huo
ulisitishwa kwa kuwa tume ya mabadiliko ya katiba ilikuwa ikikusanya
maoni kuhusu mabadiliko ya katiba. Hivyo walidhani wananchi wangetoa pia
maoni juu ya sheria hiyo lakini haikuwa hivyo. Zoezi la kukusanya maoni
ya wananchi litakamilika muda si mrefu.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni