Kurasa

Jumatano, 14 Septemba 2016

Dk. Shein aomba suluhu Z’bar


Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar

LICHA ya maneno ya kejeli kutolewa na baadhi ya viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi hao sasa wanaomba suluhu, anaandika Faki Sosi.
Zanzibar imepasuka vipande viwili kutokana na mitazamo kinzani ya kisiasa jambo ambalo limeiweka visiwa hivyo njiapanda.
Kwenye Salamu za Baraza la Eid jana visiwani Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, rais wa visiwa hivyo ameeleza kutofurahia namna wananchi walivyogawanyika.
“Hali ya kuwepo kwa mizozo kwa baadhi ya masheikh na waumini inatokana na misimamo yao, inaweza kusababisha mifarakani katika jamii,” ameeleza Dk. Shein wakati akihutubia kwenye baraza hilo lililofanyika Mkoani, Pemba.
Kumekuwepo na uhasama mkubwa visiwani humo kati ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) na CCM uliochochewa zaidi baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kinyume na Katiba ya Visiwa hivyo.
Baada ya kufuta uchaguzi huo ZEC iliitisha uchaguzi mwingine uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu uliosusiwa na CUF, tume hiyo ilimpa ushindi Dk. Shein.
Kwenye baraza hilo Dk. Shein ameeleza kuumizwa na namna mgawanyiko visiwani humo ulivyo mkubwa na kuwataka kuwa wamoja.
Ameeleza kuwa, taswira ya nchi imevurugwa na mgawanyiko visiwani humo jambo ambalo halileti afya katika maendeleo ya visiwa hivyo.
Kwenye baraza hilo ambalo viongozi wa CUF hawakuhudhuria, Dk. Shein amesema, vitendo vya kutengana vimedhihiri kwa kiasi kikubwa huku akitolea mfano wananchi kuchomeana mazao shambani.
Hata hivyo, Maalim Seif akizungumza katika Msikiti wa Kiembe Samaki, Unguja amewataka wakazi wa visiwa hivyo kuwa na subira na kwamba “hakuna jambo lisilokuwa na mwisho.”
Pamoja na Dk. Shein kutaka ‘suluhu’ ya mgawanyiko visiwani humo, serikali yake haikuipa CUF mwaliko wa kuwepo kwa baraza la pamoja la Eid kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe zilizopita.
Kauli ya kutotaka kuishirikisha CUF kwenye matukio ya kitaifa ilizungumza na CCM siku chache baada ya Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF kugomea mkono wa Dk. Shein walipokutana kwenye mazishi wa Alhaj Aboud Jumbe, Rais Mstaafu wa Zanzibar
Chanzo: Mwanahalisionline.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni