Chama cha ACT – Wazalendo kimetangaza azma yake ya kufanya
mkutano mkuu wa kidemokrasia Jumamosi ijayo licha ya kuwapo kwa amri ya
Polisi iliyokataza kufanyika kwa mikutano yote ya kisiasa nchini.
Jeshi la Polisi lilipiga marufuku maandamano na mikutano yote ya hadhara tangu Juni 7 hadi pale hali ya usalama itakapotengemaa.
Jeshi hilo lilisema limefikia hatua hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka
kwa vyama vya siasa vikitaka kufanya mikutano na maandamano kwa lengo
la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.
Lakini jana, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT –
Wazalendo, Ado Shaibu alisema wamepanga kufanya mkutano huo kwa sababu
Katiba inawaruhusu.
“ACT kimekusudia kuitisha mkutano mkuu wa kidemokrasia, hii ni haki yetu
kikatiba na hata kwa dunia nzima si ajabu kwa kuwa vyama vya siasa
hufanya hivyo. Kongamano hili litawaleta pamoja wanachama, wadau na
wafadhili wa ACT ambao watajadili hali ya maendeleo ya nchi,” alisema na
kuongeza.
“Hatutaji mahali na ukumbi tutakaoufanyia kwa sasa, wakati ukifika
tutawajulisha.Na hatutaomba kibali kwa kuwa katiba haisemi vyama vya
siasa viombe kibali vinapotaka kufanya mikutano ya ndani.”
Shaibu alisema kuwa endapo serikali itazuia kufanyika kongamano hilo
watachukua hatua za kisheria kupinga maamuzi hayo kwa madai kuwa katiba
ya nchi na ya vyama vya siasa inarushusu kufanyika.
“Serikali ilituzia kufanya mikutano na vikao vya ndani, tulikaa kimya
awali tukiamini kuwa tutaishawishi kwa hoja na itajirekebisa lakini
haikufanya hivyo.Tunaamini serikali itarudi nyuma na kuamini haina
mamlaka ya kuzuia mikutano na vikao vya ndani kwa sababu kuizuia
inamaana unafuta shughuli za siasa na sisi tutakuwa wa mwisho kukubali
vyama kufutwa ,” alisema.
Alisema ACT haitokuwa nyuma kuiunga mkono serikali inapofanya vyema na
kwamba endapo chama hicho kitakosoa utendaji kazi wake, serikali
isikichukie kwa kuwa kinatekeleza wajibu wajibu wake.
Kwa upande mwingine, Shaibu alisema Kamati Kuu ya Uongozi wa Chama cha
ACT imefanya baadhi ya marekebisho ya muundo wa uendeshaji kwa kuteua
baadhi ya makatibu wa kamati za chama hicho.
“Kikao cha tatu cha kamati kuu kilichoketi Septemba 5,2016 kilifanya
teuzi mbalimbali za makatibu, sambamba na kugawa baadhi ya kamati
ikiwemo iliyokuwa kamati ya Ulinzi, Usalama na Uadilifu ambapo kwa sasa
imegawanyika na kuwa kamati ya Usalama na Ulinzi na mpya ni Kamati ya
Uadilifu, ” alisema.
Aliwataja makatibu wapya wa kamati walioteuliwa akiwemo aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Chama cha Wananchi CUF (JUVICUF) Mohamed
Babu ambaye kwa sasa ni Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Ally
Kifu ameteuliwa kuwa Katibu wa kamati ya Fedha na Miradi ya Kujitegemea.
Katibu mwingine aliyeteuliwa ni Sabrah Mohamed ambaye ameshikilia
Kitengo cha Kushughulikia Maendeleo ya Zanzibar.
Chanzo: Muungwna blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni