WANANCHI wa Manispaa ya Bukoba, walioathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi
lililotokea Jumamosi iliyopita, wametoa ya moyoni baada ya kutaka
watendaji na wenyeviti wa mitaa mkoani Kagera, wafanye tathimini ya haki
kwa waathirika hao ili wapate takwimu sahihi zitakazowezesha kupatiwa
msaada kama ilivyolengwa.
Aidha, wamewataka watendaji na wenyeviti hao, kuhakikisha wanatoa haki
sawa kwa kila mtu aliyeguswa na janga hilo; na si kubagua kama
wanavyofanya sasa. Wananchi hao wametoa kilio chao jana mbele ya
Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdallah Bulembo ambaye alikuwa na ziara ya kukagua maeneo
yaliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuwapa pole waathirika hao.
Mkazi wa Kata ya Hamgembe Omukishenye ambaye ameathiriwa na tetemeko
hilo, Joyce Joseph ambaye nyumba yake ilianguka na kwa sasa analala nje
na familia yake ya watu saba, alimueleza Bulembo kuwa watendaji walifika
na kuangalia nyumba kwa nje, wakaandika na kuondoka.
Wananchi hao walisema wanapowaomba watendaji hao, waingie ndani waone
madhara yaliyotokea, wanajibiwa vibaya, hali inayowafanya waone kama
serikali yao imewatelekeza.
“Tunashukuru wewe kuja kutusalimia na kutuletea misaada, leo ni siku ya
tano tunalala nje, hatuna chakula, hatuna chochote tuko kama
unavyotuona. Pia tunaomba uwaagize watendaji na wenyeviti wa mitaa na
vijijini wafanye tathimini ya kina; mfano zipo baadhi ya nyumba ukipita
nje unaona nyufa, lakini ukiingia ndani kuta zote zimeanguka,
tukiwaeleza, waingie ndani wanatwambia nyamaza msitusumbue,” alidai
Joyce.
Mkazi wa Kata ya Kashai, Amoni Mwijage alisema wapo baadhi ya wenyeviti
wa mitaa, wanapopita wanabagua wakati wa kuandika majina kwa ajili ya
tathimini na wanaiendesha kisiasa.
“Kama mwenyekiti ni wa chama fulani anasema hakuna kumuandika huyu kwa
sababu si wa chama chetu, lakini wajue kuwa sisi tunaumia na wote
tunahitaji misaada na hili janga sio kwamba tuliliomba kuwa hivi. Sisi
hatuwezi kuhama maeneo yetu kwenda kwenye kambi na kuacha vifaa vyetu
watuletee mahema ya muda hapa tulipo wakati utaratibu ukiendelea wa
kutuletea msaada zaidi,” alisema Mwijage.
Baada ya Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kusikia
malalamiko hayo kutoka kwa wananchi hao aliowatembelea na kujionea hali
iliyopo, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Kamati yake ya Ulinzi na
Usalama kufanya tathimini kwa kina na kwenda ndani zaidi na kulenga mkoa
mzima, kwani waathirika hawapo Manispaa ya Bukoba tu; na endapo
hawatafanya hivyo, lawama zitakuwa kubwa na lengo lililokusudiwa
halitafikiwa.
“Watu wanaoenda kufanya tathimini na kuandika majina ya watu waingie
ndani ya nyumba, wajiridhishe ni kipi kinachoendelea sio kupita nje
wakaandika takwimu zisizo sahihi, wakati madhara ni makubwa. Pia hili
janga lisiingizwe katika mambo ya kisiasa wala itikadi fulani…hili ni
janga la Watanzania wote na ni msiba wetu sote, maana wananchi wamesema
wanabaguliwa kwa mambo ya kisiasa, hawaandikwi kwa sababu ya mtu ni
chama fulani, alisema Bulembo.
Aidha, Bulembo alitoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo vyandarua, kilo
500 za mchele, maji ya kunywa, chumvi, shuka, maharage kilo 250 na
mablanketi vyenye thamani ya Sh milioni 6.8, na Sh milioni mbili taslimu
kukarabati Shule ya Sekondari ya Omumwani, inayomilikiwa na Jumuiya ya
Wazazi Bukoba Mjini. Fedha zote ni Sh milioni 8.8.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema taarifa za sasa kuhusu hali
ilivyo ikiwamo nyumba zilizoathirika, zikiwemo zilizoanguka 840 na
zenye nyufa kubwa 1,264 ilikuwa ya awali, lakini tathimini inaendelea na
mpaka sasa inakadiriwa nyumba 5,000 zimeathiriwa na tukio hilo, ambalo
halijawahi kutokea Tanzania.
Kijuu alisema majeruhi wamepungua na kubaki 51 kati ya 170 waliokuwa
amelazwa, ambao 23 kati ya hao wanahitaji kufanyiwa upasuaji.
“Lakini bado wananchi wanalala nje hatujapata mahema, kwa sasa wataalamu
wa jiolojia watapita mitaa yote ili kutoa elimu kwa wananchi ili waweze
kujikinga vipi pale wanapohisi hali kama hiyo, pia Ubalozi wa China
umeagiza dawa, ziko njiani zinaletwa kwa ajili ya waathirika hao,”
alisema Kijuu na kuongeza:
“Kwa hatua za mwanzo tunapanga kuwapatia wananchi kila familia bati 20
na mifuko mitano ya saruji huku wapangaji walioathirika watapewa
shilingi 120,000 kwa ajili ya kulipia kodi kwa muda wa miezi sita. Pia
mpaka sasa wapo madaktari 13 wa kawaida kutoka Hospitali ya Rufaa ya
Kanda Bugando, madaktari bingwa watano wakiambatana na mkurugenzi wa
hospitali hiyo ya rufaa, wataalamu wa usingizi wawili, madaktari wa
upasuaji wanne, muuguzi wa kawaida mmoja na madaktari sita kutoka
China.”
Misaada mbalimbali imeanza kutolewa, kwa wabunge kutoa posho yao ya siku
moja huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akichangisha zaidi ya Sh bilioni
1.4 kutoka kwa Jumuiya ya Mabalozi na wafanyabiashara nchini kwa ajili
ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia nchini, Profesa Abdukarim Mruma
alisema tangu Tanzania ipate Uhuru, hili ni tetemeko la tisa kutokea
lakini mengine yalikuwa madogo, tofauti na la Jumamosi, kwani wamefanya
utafiti na kugundua kitovu cha tetemeko hilo ni wilayani Missenyi katika
Msitu wa Minziro.
“Hatuna chombo cha kutabiri matetemeko kabla ya kutokea dunia nzima
hakuna kipimo hicho, hatumung'unyi maneno matetemeko yatazidi kutokea,
lakini madogo ila tulichogundua ni kwamba Kagera iko karibu na Bonde la
Ufa na pia miamba iliyoko chini ni laini ukilinganisha na Mkoa wa Mwanza
kwa hiyo inasababisha tetemeko likitokea hata dogo lazima lilete
madhara fulani,” alieleza Profesa Mruma.
Aliwashauri wananchi kuacha kukimbia nyumba zao pindi wanapoona au
kusikia dalili ya tetemeko hilo, bali waingie uvunguni mwa meza, vitanda
au katika kingo za nyumba ambako wanakuwa salama zaidi kwani tetemeko
linachukua sekunde zisizozidi nane kupita wakati watu wakikimbia
wanakutana na kuta au milango inayowadhuru.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni