POLISI mkoani Morogoro inamshikilia Anna Luambano (33) ambaye ni mkazi
wa Kipawa jijini Dar es Salaam kuwa tuhuma za wizi wa mtoto, Angel Meck
mwenye umri wa siku 10 baada ya kumlaghai mama wa mtoto huyo, Maimuna
Mahamudu (20) mkazi wa Chamwino katika Manispaa ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei amesema wizi huo ulitokea
Septemba 13, mwaka huu saa 5 asubuhi katika Mtaa wa Kilimahewa Manispaa
ya Morogoro.
Akielezea mazingira ya wizi huo, Kamanda Matei amesema mtuhumiwa
alimdanganya mama wa mtoto huyo wakiwa njiani kutoka Kituo cha Afya
Mafiga, akimwomba ampe mtoto wake akamwoneshe mume wake kuwa huyo ni
mtoto wa mdogo wake, ambaye amejifungua ili awape fedha za hongera na
kisha wagawane.
Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kupewa mtoto huyo, alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Baada ya mama wa mtoto kutambua mwanawe ameibwa, alienda kutoa taarifa Kituo cha Polisi kutoa taarifa ya wizi huo.
Amesema Polisi baada ya kupata taarifa hiyo, walifanya msako kwenye
mabasi ya abiria yanayosafiri maeneo mbalimbali, na kufanikiwa kumkamata
mtuhumiwa akiwa katika basi la Upendo eneo la Mdaula mkoani Pwani
akienda jijini Dar es Salaam.
“Polisi bado inaendelea kumhoji kuhusiana na tukio hilo na hatua za kumfikisha mahakamani zinafuata,” amesema Kamanda Matei.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Kamanda wa Polisi
Mkoa, mtuhumiwa Anna alidai hakuwa na nia mbaya ya kumwiba mtoto huyo,
bali ni kumtunza kwa kuwa hana mtoto.
“Sijabahatika kuzaa mtoto wala sijaolewa na nimehangaika kupata mtoto wa
kumleta hadi kufikia hatua ya kuomba mtoto Ustawi wa Jamii lakini
sijafanikiwa. Nami ninapenda niwe na mtoto wa kumlea na kuishi naye,
nikaamua nimchukue huyu mtoto,” amesema mwanamke huyo.
Kwa upande wake, mama wa mtoto huyo alithibitisha mbele ya mwandishi wa
habari hizi nje ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa kuhusu kuibwa
mwanawe huyo akiwa njiani akitoka Kituo cha Afya cha Mafiga alipokuwa
amejifungulia.
Alisema alikuwa hamfahamu mwanamke huyo wala makazi yake, isipokuwa
walikutana njiani, yeye akitoka eneo hilo la Mafiga kurejea nyumbani
kwao na hakuweza kuendelea kuelezea kwa kina kisa hicho, isipokuwa
kulishukuru Jeshi la Polisi kuwezesha kupatikana kwa mwanawe.
Tukio hilo la wizi wa mtoto mchanga ni la pili kufanywa na wanawake wa
kutoka Dar es Salaam kwani Agosti mwaka huu, Polisi Morogoro
iliwashikilia wanawake wawili wakazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam,
Sarafina Henry (28) na Johari Hussein (22) kwa tuhuma za wizi wa mtoto
wa kike.
Mtoto huyo aliibwa kutoka kwa wenye mtoto, Ashura Shabani (33) mtaa wa
Karume, Manispaa ya Morogoro akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu mwaka
2013. Alipatikana Agosti 7, mwaka huu akiwa ametimiza umri wa miaka
minne na nusu huku watuhumiwa wakimwandaa kumwanzisha kusoma elimu ya
awali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni