MSUKUMO wa kuandika makala hii ni baada ya maombi ya wasomaji na watumiaji wa mtandao wa WhatsApp.
Ni kweli kwamba kwasasa kuna mambo mengi ambayo yanaendelea mitandaoni zikiwamo taarifa zinazosambazwa juu ya mpango wa WhatsApp kutaka kutumia taarifa zako Facebook.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, WhatsApp walitangaza kutaka kushirikishana taarifa (data) na Facebook.
Taarifa hizo za watumiaji wa WhatsApp zitatumiwa kuvutia matangazo yanayoonekana na watumiaji wa mtandao wa Facebook.
Hii ikimaanisha nambari za simu na maelezo ya mara ya mwisho mteja kuingia katika akaunti yake ya WhatsApp na Facebook.
Hata hivyo mara baada ya kuwapo kwa mpango huo, WhatsApp ilitoa muda wa siku 30 kwa ajili ya wateja wake ambao hawako tayari waweze kujiondoa kwenye huduma hii.
Kwasasa kama bado hujapata ombi kutoka WhatsApp la kukataa au kukubali kwa maana ya (Terms and Privacy Policy) ambayo ni mpya kutoka WhatsApp basi tarajia kupata muda wowote kabla ya mwezi kuisha.
Kwa mtazamo wa haraka unaweza kuona kwamba hakuna njia ya kukataa kile kinachopendekezwa na mtandao huu, lakini kuna namna ambayo unaweza kufuata na kuepukana na huduma hii jambo ambalo WhatsApp wanatambua fika kuwa si rahisi kwa watumiaji wake kulifanikisha.
Kwanza kabisa unapofungua akaunti yako ya WhatsApp bofya upande wa juu kulia kisha chagua ‘Settings’ ikifuatiwa na Account (alama ya ufunguo) kisha utaona ujumbe unaosema Share My Accout. Endapo utakubaliana na maelezo hayo utakuwa umeruhusu taarifa zako za WhatsApp kutumika Facebook.
Hivyo inakubidi ubonyeze kwenye kitufe cha alama ya ‘tiki’ ili uweze kukataa taarifa zako kutumiwa kwani tayari WhatsApp wameshaweka tiki hiyo kwa maana kwamba umekubali kwa taarifa zako kutumiwa Facebook.
Tambua WhatsApp wameweka muda wa siku 30 pekee za mtumiaji kukataa kujiunga na huduma hiyo, hujachelewa kwani bado kuna siku chache kabla ya utaratibu huo kufikia kikomo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni