Kurasa

Ijumaa, 23 Septemba 2016

Maiti wahifadhiwa chini kwa uhaba wa majokofu

WAKAZI wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, wameitaka serikali kuiangalia kwa jicho la huruma hospitali ya wilaya hiyo kutokana na uhaba wa majokofu ya kuhifadhia maiti.

Kwa mujibu wa wananchi hao, hatua hiyo imesababisha maiti kuharibika mapema.

Vilevile,  chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo ni kidogo ikizingatiwa  hospitali hiyo inahudumia wakazi wengi.

Wakizungumza na MTANZANIA juzi, walisema licha ya hospitali hiyo kuwa na  majokofu machache lakini yaliyopo pia ni mabovu.

Issa Mwahu,  mmoja wa wakazi wa wilaya hiyo, alisema iko haja kwa serikali kuliangalia suala hilo kwa makini kwa vile  watumishi hospitalini hapo wanalifanya   siri suala hilo.

“Unaweza kufikiri ndugu yako amehifadhiwa katika friji kumbe hajawekwa na hii ni kwa sababu mafriji hayo ni machache. Tunaiomba serikali iliangalie jambo hili,” alisema Mwahu.

Akizungumzia hali hiyo, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Rashid Ikaji alisema habari hizo ni za uzushi.

“Suala hilo halina ukweli wowote, mafriji yapo vizuri hakuna maiti iliyowahi kuharibika sababu ya kutowekwa katika friji wanaokwambia hivyo usiwasikilize,” alisema.

Dk. Ikaji alisema changamoto wanayokabiliwa nayo ni moja tu ambayo ni udogo wa majengo hasa la maabara ambalo linahitaji kupanuliwa.
Chanzo:Muungwana blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni