Kurasa

Ijumaa, 16 Septemba 2016

Jifunze KuandikaHabari kwenye mtandao kupitia bbcswahili

Tunahitaji kuzifanya ripoti ziwe fupi kwa sababu ni taabu zaidi kusoma kwenye skrini, au kwenye simu ya mkono kuliko kusoma kwenye karatasi. Aghalabu, hutakiwi utoe maelezo mengi katika ripoti zako.

Mvutie msomaji
Msomaji wa mtandao ni kiumbe aliye na kigeugeu. Watauchungua ukurasa kutafuta habari na wasipokiona kwa haraka wanachokitafuta wataacha na kusonga mbele, yumkini wakautafuta mtandao mwingine.  Kwa hivyo wape wanachokihitaji mwanzoni mwa ripoti. Fikiria namna utavyomueleza mtu habari akiwa katika mahala palipojaa watu na penye kelele — sentensi gani utazozitumia kuieleza ripoti yako? Aghalabu hiyo huwa ibara ya mwanzo ya ripoti yako.
Vichwa vizuri vya habari
Msomaji ataupitia ukurasa wa mwanzo kutafuta habari na kichwa kizuri cha habari kitamwambia ripoti hiyo ni kuhusu nini, hivyo hatovunjika moyo akibonyeza na kuona kwamba ni kuhusu jambo asilolitarajia.
Zifanye ripoti zako ziwe fupi
Tunahitaji kuzifanya ripoti ziwe fupi kwa sababu ni taabu zaidi kusoma kwenye skrini, au kwenye simu ya mkono kuliko kusoma kwenye karatasi. Aghalabu, hutakiwi utoe maelezo mengi katika ripoti zako. Maelezo hayo tayari yanapatikana katika ripoti nyingine tulizokwishaziandika na tunaweza kumuongoza msomaji azipate ripoti hizo ikiwa atataka maelezo zaidi. Ikiwa ripoti yako ina nyanja nyingi basi fikiria kuigawa kwa mafungu ili msomaji wako aweze kuyasoma kwa urahisi.
Ifanye ripoti yako itoe picha halisi
Katika vyombo vingine vya habari kama televisheni au redio unaweza ukawasikia au kuwaona watu wanaozungumzwa katika ripoti yako. Ripoti ya maandishi ni tofauti. Ni lazima uwafanye watoe picha halisi ya mambo yalivyo na njia moja nzuri ya kufanya hivyo ni kutumia maneno waliyoyasema wenyewe. Kwa hivyo ingiza dondoo za kusisimua katika ripoti zako, dondoo ambazo zitabainisha kitu au jambo kuhusu mtu anayezungumzwa kwenye ripoti na usiogope kuingiza katika ripoti yako maelezo yatayoifanya ripoti isisimue kwa kutoa picha halisi.
Iandike tena ripoti yako
Tunalenga kuungana na watu na kuwaeleza tunayotaka kuyasema kwa njia itayofahamika kwa urahisi iwezekanavyo.  Kumbuka kwamba kila ripoti hufaidika ikiandikwa tena, kwa mara nyingine, ikiwa unao wakati.  Na usitaraji kwamba makosa ya sarufi au ya tahajia yataweza kuonekana kabla ya ripoti yako kuchapishwa. Wasomaji wanachukizwa wakiona tunakosea katika mambo ya msingi na hawachelewi kutwambia.
Namna ya kuipanga ripoti kwenye ukurasa
Ukiwa mwandishi, kuna fursa nzuri kwamba utaamua jinsi ripoti yako itavyoonekana kwenye ukurasa.  Unaweza ukaandika ripoti ya kusisimua, lakini ikiwa itachapishwa kama kipande kimoja msomaji hatovutiwa nayo. Tumia picha nzuri, michoro, visanduku vyenye maelezo, dondoo…
Kutumia vyombo vingine vya habari
Je, kuandika maneno elfu moja ndo njia bora ya kueleza ripoti yako kwenye mtandao? Pengine njia bora ya kufanya hivyo ni kutumia picha, video au sauti. Ikiwa ripoti yako inamchochea msomaji atafakari, basi huenda ikahitaji pawepo pia na sauti.  Hiyo ni moja ya faida kubwa za mtandao: kuweza kutumia vyombo tofauti vya habari kuelezea ripoti.
Changanua ripoti nzuri
Angalia jinsi mtandao wa Habari wa BBC na mitandao mingine inavyoandika ripoti zao. Tafuta ripoti ambazo unahisi ni nzuri na zichanganue ili uweze kujua kwa nini ni nzuri. Angalia nini wasomaji wanachotafuta katika mtandao.  Kuna takwimu nyingi juu ya nini kinachopendwa na kipi kisichopendwa. Unaweza kujifunza mengi kutokana na haya

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni