.
Wakimbizi wa Somalia kutoka Kenya wanapewa taarifa zisizo sahihi ambazo
zinawasabishia taharuki huku watetezi wa haki za binadamu wakisema
mpango huo haukidhi viwango vya kimataifa
Wakimbizi katika kambi ya Daadab Kaskazini Mashariki mwa Kenya
Wakimbizi katika kambi ya Daadab Kaskazini Mashariki mwa Kenya
Taarifa za kufungwa kwa kambi ya wakimbizi ya Daadab zimezusha wasiwasi mkubwa na huenda hatua hiyo ikawatumbukiza tena wakimbizi kwenye hali ya hatari.
Takriban wakimbizi 263,000 kutoka Somalia wanaishi katika kambi hiyo ya Daadab ambayo ndiyo imekuwa makaazi yao tangu walipotoroka machafuko nchini mwao.
Katika mwezi Mei mwaka huu serikali ya Kenya ilitangaza azma yake ya kuharakisha kuwarudisha kwao wakimbizi wa Kisomali na hatimae kuifunga kambi ya wakimbizi ya Daadab iliyo kaskazini mashariki mwa
Kenya ifikapo mwezi Novemba mwaka huu. Baadhi ya wakimbizi wamesema wamekubali kurudi nchini mwao kwa hiari kwa kuogopa labda serikali ya Kenya itawarudisha kwa lazima endapo wataendelea kuishi katika kambi hiyo.
Wakimbizi wa Kisomali wakichunga wanyama wao katika kambi ya Dagahaley nje ya kambi ya Daadab
Wakimbizi hao wameeleza kuwa sababu zote hizi zimewafanya wakubali kurudi nchini Somalai ambako wanakabiliwa na hatari, mateso na njaa.
Sheria inayowalinda wakimbizi inakataza kuwarudisha makwao kwa lazima
Babatunde Olugboji,naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch amesema, serikali ya Kenya haiwapi wakimbizi wa Somalia nafasi ya kujichagulia iwapo wanataka kuendelea kuishi nchini humo au kurudi Somalia na wakati huo huo shirika linalosimamia wakimbizi la Umoja wa Mataifa haliwapi wakimbizi hao taarifa kamili kuhusiana na hali ya usalama nchini Somalia.
Makubaliano ya hali ya wakimbizi ya mwaka 1951 yanakataza kuwarudisha wakimbizi kwa nguvu katika sehemu ambapo uhuru na usalama wao unatishiwa. Shirika la kutetea haki za kibinadamu limewahoji takriban wakimbizi 100 pamoja na wale waliofanya maombi ya hifadhi ya kisiasa.
Wakimbizi hao wa Somalia wamesema uamuzi wa serikali ya Kenya wa kuifunga kambi ya wakimbizi ya Daadab umewatia mtegoni na kwamba wanaogopa kurudi nchini mwao Somalia.
Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR nchini Somalia limewaeleza wachunguzi wa haki za binadamu kuwa hali katika Somalia ya kati si shwari na kwamba haliko tayari kuwapokea wakimbizi kwa sababu watu wa eneo hilo wanaendelea kukabiliwa na hali ngumu kutokana na machafuko yanayoendelea.
Mwandishi: Zainab Aziz
Mhariri: Gakuba Daniel
Chanzo:DW
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni