Kurasa

Jumatatu, 12 Septemba 2016

Ukawa Waendeleza Mgomo Dodoma

 



Dodoma. Wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamesusia mechi ya mpira wa mguu kati ya timu ya wabunge na Kamati ya Amani ya viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa madai kuwa kuna ajenda ya siri kwenye mchezo huo.

Kutokana na uamuzi huo, badala ya viongozi hao wa dini kucheza na timu ya Bunge, walicheza timu ya maveterani ya Dodoma huku taarifa nyingine zikidai kuwa wabunge wamezuiwa kushiriki.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Dodoma juzi, wabunge wa Ukawa walisema wameacha kwenda kucheza baada ya kutoshirikishwa katika maandalizi ya mechi hiyo.

Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga alisema hawakuenda uwanjani kwa sababu kamati hiyo ilialikwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ambaye wamekuwa na mgogoro naye kwa muda mrefu.

Katika Bunge la Bajeti, wabunge wa Ukawa waliingia katika mgogoro na Dk Tulia uliowafanya kususia vikao vilivyoendeshwa naye kwa madai ya kuwapo kwa ukiukwaji wa demokrasia.

“Tuliona mambo yaliyojificha ndani ya mechi hiyo ndiyo maana hatukuenda uwanjani. Hatuwezi kuharibu mazungumzo mazuri yaliyopo kati yetu na viongozi wa dini na ndiyo maana hatukuenda huko,” alisema Haonga.

Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali pia alisema hawakuenda kushiriki katika mchezo huo kwa sababu hawakushirikishwa katika maandalizi.

Alisema ziara hiyo ililenga kurejesha mshikamano ndani ya Bunge, suala ambalo viongozi wa dini wa kitaifa washalibeba na kuahidi kwenda kuzungumza na Rais John Magufuli.

“Timu uliyokuja kucheze nasi ilikuja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye katika mkoa wake alishindwa kuwatambulisha kwa Rais, madiwani, mbunge na meya. Ashughulike na matatizo yake ya Dar es Salaam,” alisema.

Hali uwanjani
Katika Uwanja wa Jamhuri, Dk Tulia alionekana akiwa na wabunge wachache waliokuwa wakitazama mpira huo tofauti na michezo mingine inayofanyika katika uwanja huo.

Katika timu hiyo ya maveterani, aliingia mbunge mmoja tu wa Makete (CCM), Dk Norman Sigalla na baadhi ya wakazi wa Dodoma waliofika uwanjani walisikika wakihoji walipo wachezaji maarufu wa timu hiyo ya Bunge.

Wachezaji waliotajwa ni Ridhiwani Kikwete (Chalinze-CCM), Mwigulu Nchemba (Waziri wa Mambo ya Ndani), Antony Mavunde (Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana na Ajira), Sadifa Khamis Juma (Donge-CCM) na Naibu Waziri wa Afya, Dk Khamis Kigwangalah.

Mwenyekiti wa Timu ya Bunge, Willam Ngeleja alipotafutwa simu yake iliita bila majibu.
Hata hivyo, siku moja kabla ya kuchezwa kwa mechi hiyo Ngeleja alikaririwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) akisema mchezo huo ulilenga kuenzi amani kwa Watanzania.

Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Ester Matiko alisema alitingwa na shughuli za mahafali ya mtoto wake hivyo hakuweza kufuatilia kujua ni kwa nini timu ya Bunge haikucheza.

“Sijajua lengo la mechi lakini kama ni kupatanishwa kwa kutumia timu hiyo sidhani kama ingesaidia kwa sababu (Ukawa) hatufiki hata wabunge 10 kwenye timu,” alisema.

Dk Tulia alisema wabunge wengi hawakuwepo katika mechi hiyo kwa sababu ni mwisho wa wiki na wengine wameenda mashambani na wengine majimboni.
Chanzo Mungwanablog.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni