Manchester, England. Kocha Jose Mourinho amemshutumu mwamuzi Mark
Clattenburg kwa kuinyima Manchester United penalti mbili za wazi
wakinyukwa mabao 2-1 na Manchester City kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Mourinho alijiridhisha kuwa mwamuzi Clattenburg alitakiwa kumtoa kipa
Claudio Bravo kwa kadi nyekundu na kuipa Manchester United penalti baada
ya kipa huyo wa Manchester City kumchezea vibaya Wayne Rooney kipindi
cha pili, huku pia mwamuzi akikataa kuipa Manchester United penalti
nyingine wakidai Nicolas Otamendi alinawa mpira. “Tumeumizwa na Mark kwa
uamuzi wake mbaya wa kipindi cha pili,” alisema Mourinho.
“Najua sheria za mchezo huu. Bila ubishi ile ilikuwa penalti na kadi
nyekundu kwa Bravo. Kama ni nje ya eneo la hatari, ingekuwa ni mkwaju wa
adhabu na kadi nyekundu. “Kulikuwa na uwezekano mkubwa wa mchezo
kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 muda mrefu, lakini kwa sasa
tunazungumza kitu kingine.”
Mourinho pia aliwashukia baadhi ya wachezaji wake Jesse Lingard, Henrikh
Mkhitaryan na Paul Pogba akidai kuwa walikuwa wakicheza kwa uwezo
binafsi zaidi na kukataa kufuata maelekezo yake.
“Niliwaambia walipokuwa mapumziko kuwa baadhi yao wanajaribu kufanya
mambo ambayo niliwakataza, walikuwa wakicheza kwa uwezo binafsi zaidi,”
aliongeza kocha huyo wa Ureno.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni