Kurasa

Ijumaa, 23 Septemba 2016

Siri ya kuruhusu mikutano ya siasa yatajwa

SIKU moja baada ya Nsato Marijani, Kamishina wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi hapa nchini, kutangaza ruhusa ya kufanyika kwa mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kuna jambo limejificha nyuma ya ruhusa hiyo

Jeshi la Polisi kupitia Kamishina Marijani, tarehe 24 Agosti mwaka huu, lilipiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa, ikiwemo ile ya ndani lakini siku ya jana limetangaza kuiruhusu mikutano hiyo.


“Tumeamua kuruhusu mikutano ya ndani ya vyama vya siasa na ile ya hadhara ya wabunge kwasababu, tumejiridhisha kuwa hali ya kiusalama kwa sasa ni shwari kabisa ndani ya nchi yetu,” alisema jana Nsato Marijani, Kamishina wa Operesheni na Mafunzo ya polisi.

Akieleza namna Chadema ilivyopokea ruhusa hiyo, Salum Mwalimu, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho taifa, amesema wamelipuuza tamko hilo kama walivyofanya katika tamko la awali lililotolewa na jeshi hilo.

“Walipopiga marufuku, sisi tulipuuza marufuku hiyo na tuliendelea na vikao vya ndani kwasababu tuliona amri yao haina mashiko kisheria. Lakini tunazo taarifa kuwa polisi wameruhusu mikutano hiyo kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaanza vikao vyake hivi karibuni,” amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, amesema, “Tuna taarifa kuwa, CCM imepanga kuanza vikao vyake vya ndani hivi karibuni, ndiyo maana mliona hata Rais John Magufuli alipotembelea Uhuru Media Group, alipotaka kufanya baadhi ya maamuzi Abdurahman Kinana, alinukuliwa akisema maamuzi hayo yatafanywa na vikao vya chama.”

Mwalimu amesema kuwa, CCM kufanya mikutano yao ya ndani na hata ya hadhara ni haki yao ya kikatiba na kisheria, lakini inasikitisha polisi kupiga marufuku mikutano inapofanywa na wapinzani na kuruhusu kila CCM wanapotaka kuanza kuifanya.

“Polisi wameruhusu mikutano ili CCM itakapoanza vikao vyake vya ndani isionekane kuwa wanakiuka maagizo ya Jeshi la Polisi, walifanya hivyo hata kipindi cha nyuma, walifungia vikao vyote na mikutano ya vyama lakini ulipokaribia mkutano mkuu wa CCM wakaruhusu vikao vya ndani.

Msishangae baada ya CCM kumaliza vikao vyake vya ndani wiki mbili zijazo, polisi wakajitokeza tena na kusema hali ya usalama imekuwa tete na wakatangaza kuzuia tena mikutano ya ndani ya vyama vya siasa. Tunaonya na kulaani tabia hii ya polisi kutumika kisiasa,” amesema Mwalimu.

Katika hatua nyingine Chadema imepongeza hatua ya Rais Magufuli na Mwenyekiti wa CCM kuamuru wizara na taasisi zote za serikali zinazodaiwa na vyombo vya habari vya Uhuru vilipe madeni hayo haraka iwekanavyo. Hata hivyo chama hicho kimetoa angalizo kikisema;
“Rais anaweza kuwa na nia njema kabisa kuamuru serikali anayoiongoza ililipe Uhuru ambalo pia ni mali ya chama anachokiongoza, lakini si Uhuru pekee wanaoidai serikali bali vipo vyombo vingi vya habari vinavyoidai serikali fedha nyingi pia.

Rais Magufuli kama ana nia njema, aagize wizara na taasisi zote za serikali zilipe madeni yote wanayodaiwa na vyombo vyote vya habari kwani vipo vingi vinavyoidai serikali na waandishi wanafanya kazi katika mazingira magumu. Rais ni baba wa wote, atende haki kwa wote.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni