Kurasa

Jumatano, 14 Septemba 2016

Rais Dkt. Magufuli Amuapisha Balozi Dk. Dau Pamoja Na Makatibu Tawala Wa Mikoa Mitatu Ikulu Jijini Dar Es Salaam.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 14 Septemba, 2016 amemuapisha Dkt. Ramadhani Kitwana Dau kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi, Dkt. Ramadhan Kitwana Dau alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF)

Mhe. Balozi Dkt. Ramadhani Kitwana Dau anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Dkt. Aziz Ponary Mlima ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amewaapisha Makatibu Tawala wa Mikoa mitatu aliowateua mwishoni mwa wiki iliyopita.

Walioapishwa ni  kwanza, Bw. Eliya Mtinangi Ntandu anayekuwa Katibu Tawala wa kwanza wa Mkoa wa Songwe ulioanzishwa rasmi Mwezi Februari 2016.

Pili, Bw. Adoh Stephen Mapunda anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara.

Bw. Adoh Stephen Mapunda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Benedict Richard Ole Kuyan ambaye amestaafu.

Tatu, Bw. Tixon Tuliangine Nzunda anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa.

Bw. Tixon Tuliangine Nzunda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Symthies Emmanuel Pangisa ambaye amestaafu.

Baada ya kuapishwa, Mhe. Balozi Ramadhani Kitwana Dau na Makatibu Tawala wote watatu wamekula Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na kushuhudiwa na Rais Magufuli.

Matukio yote yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
14 Septemba, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Bw. Tixon Nzunda kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Bw. Eliya Ntandu kuwa Katibu Tawala mkoa wa Songwe, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Malaysia Dkt. Ramadhani Dau mara baada ya tukio la uapisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
 


Advertisement
==

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni