Kijana Saidi Mnyambi (26) anayedaiwa kung’atwa 1/3 ya ulimi wake
wakati wakinyonyana ulimi na mwanamke mmoja, ameingiwa na hofu kuwa
mchumba wake anaweza kumwacha kutokana na kitendo hicho.
Kijana huyo mkazi wa Unyankhae, Manispaa ya Singida, aliyasema hayo juzi hospitalini alikolazwa .
Alisema hofu aliyonayo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na tukio hilo kuwa gumzo kubwa ndani na nje ya Singida.
“Kabla ya tukio hilo, uchumba wangu ulikuwa unaendelea vizuri na mambo
yalikuwa yanaelekea kwenye kufunga ndoa lakini sasa nina hofu mwenzangu
anaweza akapotoshwa na mambo yakaharibika. Nikitoka hospitalini
nitalifuatilia jambo hili kwa ukaribu zaidi ili kuweka mambo sawa,”
alisema Mnyambi.
Kuhusu matibabu, Mnyambi alisema anaendelea vizuri na kwamba sasa anaongea vizuri kama binadamu wengine na maumivu yamepungua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Peter Kakamba alisema wanamshikilia
mwanamke huyo (jina hajalitaja) aliyemng’ata ulimi Saidi na wanaendelea
na upelelezi kabla sheria hazijachukua mkondo.
Alisema mkuu wa upelelezi makosa ya jinai Mkoa wa Singida anakamilisha
uchunguzi lakini akabainisha kuwa taarifa zilizoenea awali kuhusu tukio
hilo ni tofauti na hali halisi.
“Baada ya kumpata mwanamke anayetuhumiwa kumng’ata ulimi Mnyambi,
zimepatikana taarifa mpya. Waandishi kuweni na subira tutawapatia
taarifa zenye mashiko wakati wowote kuanzia sasa,” alisema Kakamba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni