RAIS
John Magufuli amesema Serikali itarekebisha miundombinu iliyoharibika
mkoani Kagera kutokana na tetemeko la ardhi la wiki iliyopita, lakini
akawataka waliobomokewa nyumba, wajipange kuzirekebisha.
Taarifa
ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, imeeleza kuwa Rais
Magufuli alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam, wakati akipokea taarifa
ya maafa yaliyosababishwa na tetemeko hilo, kutoka kwa Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa iliyoeleza kuwa tayari Sh bilioni 3.6 zilikuwa
zimekusanywa.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Magufuli alisema Serikali pekee
yake haitaweza kujenga nyumba zote zilizobomoka, ambazo taarifa ya
Waziri Mkuu ilisema zilizobomoka ni 2,063; zilizo kwenye hali hatarishi
14,081 na zilizopata uharibifu mdogo ni nyumba 9,471.
Madhara
mengine yaliyotokea ni pamoja na vifo vya watu 17 na majeruhi 440 huku
watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.Kuhusu miundombinu
iliyoharibika, Rais Magufuli alisema Serikali itarekebisha shule, vituo
vya matibabu, barabara na huduma nyingine za kijamii.
Pamoja
na kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli amepokea mchango wa fedha
taslimu Dola za Kimarekani 200,000, sawa na takribani Shilingi za
Kitanzania milioni 437, kutoka kwa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta
Museveni.
Mbali
na msaada huo, pia amepokea taarifa ya mchango wa mabati, blanketi na
magodoro vyenye thamani ya Sh milioni 115 kutoka kwa Rais wa Kenya,
Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.
Rais
Magufuli aliwashukuru wote waliojitoa kusaidia waathirika akiwemo Rais
Museveni wa Uganda; Rais Kenyatta wa Kenya na Rais Paul Kagame wa
Rwanda, ambao wamempigia simu za kumpa pole na tayari wametoa misaada
yao.
Pia
alishukuru nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa
umma na watu binafsi na kuongeza kuwa michango hiyo ina umuhimu mkubwa,
katika kukabiliana na athari za maafa hayo.
Aidha,
Rais Magufuli amewasihi Watanzania kupuuza watu wanaotaka kutumia maafa
haya kueneza chuki dhidi ya Serikali na ameweka wazi kuwa mpaka sasa
hakuna teknolojia ya kutabiri tetemeko la ardhi na hilo halikuletwa na
Serikali.
Dk
Magufuli amesema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi
na teknolojia, yamekuwa yakikumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha
vifo vingi na uharibifu mkubwa wa mali.
“Nilikuwa
najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China mwaka 2014; watu 617
walipoteza maisha, mwaka 2013 walipoteza maisha watu 193, mwaka 2010
walipoteza maisha watu 2,998 na mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712.
“Ukijaribu
kuangalia Japan, nchi iliyoendelea na ina utaalamu wa hali ya juu sana,
kwenye mwaka 2016 April 14, ilipoteza watu sita, baada ya siku mbili,
Aprili 16, 2016 tetemeko likatokea tena na likaua watu 35.
“Mwaka
2012 likaua watu 3, mwaka 2011 likaua watu 15,904 mwaka 2008 likaua
watu 12, mwaka 2007 likaua watu 11, mwaka 2004 liliua watu 40 na mwaka
1923 liliua watu 142,800 na hiyo ni Japan,” alisema.
Katika
taarifa yake, Waziri Mkuu alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali,
ikiwemo kupeleka chakula, huduma za matibabu na hifadhi za dharura kwa
waathirika na imeratibu ukusanyaji wa michango kutoka sehemu mbalimbali.
Hafla
hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga na Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.
Chanzo: Ubuyublog.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni